Mlango 27
1 Ndipo Daudi aliposema moyoni mwake, Siku moja, basi, mimi nitaangamia kwa mkono wa Sauli; hakuna jema zaidi kwangu kuliko kukimbia mpaka nchi ya Wafilisti; naye Sauli atakata tamaa kwa habari yangu, asinitafute tena mipakani mwote mwa Israeli; hivyo nitaokoka katika mikono yake.
2 Basi Daudi akaondoka, yeye na hao watu mia sita aliokuwa nao, akamvukia Akishi, mwana wa Maoki, mfalme wa Gathi.
3 Daudi akakaa huko Gathi pamoja na Akishi, yeye na watu wake, kila mtu na watu wa nyumbani mwake; Daudi naye alikuwa na wakeze wawili, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili wa Karmeli, aliyekuwa mkewe Nabali.
4 Naye Sauli akaambiwa ya kwamba Daudi amekimbia mpaka Gathi; wala hakumtafuta tena.
5 Daudi akamwambia Akishi, Sasa kama nimeona kibali machoni pako na nipewe mahali katika miji hii mmojawapo mashambani, nipate kukaa huko; mbona mtumwa wako akae katika mji wa kifalme pamoja na wewe?
6 Ndipo Akishi akampa Siklagi siku ile; kwa sababu hiyo huo mji wa Siklagi ni mali ya wafalme wa Yuda hata hivi leo.
7 Na hesabu ya siku alizokaa Daudi katika nchi ya Wafilisti ilikuwa mwaka mzima na miezi minne.
8 Naye Daudi na watu wake walikuwa wakikwea na kuwashambulia Wageshuri, na Wagirizi, na Waamaleki waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo, tangu Telemu, hapo uendapo Shuri, hata mpaka nchi ya Misri.
9 Tena Daudi akaipiga nchi hiyo, asimhifadhi hai mume wala mke, akateka nyara kondoo, na ng'ombe, na punda, na ngamia na mavazi; kisha akarejea na kufika kwa Akishi.
10 Naye Akishi humwuliza, Je! Mmeshambulia upande gani leo? Na Daudi husema, Juu ya Negebu ya Yuda, au, juu ya Negebu ya Wayerameeli, au, juu ya Negebu ya Wakeni.
11 Tena Daudi hakumhifadhi hai mume wala mke, ili kuwaleta Gathi maana alisema, Wasituchongee kusema, Ndivyo alivyofanya Daudi, tena ndivyo ilivyokuwa desturi yake wakati wote alipokaa katika nchi ya Wafilisti.
12 Hivyo Akishi akamsadiki Daudi, akasema, Amewachukiza kabisa hao watu wake Israeli; kwa hiyo atakuwa mtumishi wangu hata milele.