Mlango 14
1 Basi ikatukia siku moja, ya kwamba Yonathani, mwana wa Sauli, akamwambia yule kijana aliyemchukulia silaha zake, Haya! Na tuwavukie Wafilisti ngomeni, pale ng'ambo ya pili. Walakini hakumwarifu babaye.
2 Naye Sauli alikuwa akikaa katika upande wa mwisho wa Giba, chini ya mkomamanga ulioko kwenye uga; na hao watu waliokuwa pamoja naye walipata watu mia sita;
3 na Ahiya, mwana wa Ahitubu nduguye Ikabodi, mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa Bwana huko Shilo, mwenye kuvaa naivera. Tena hao watu hawakujua ya kwamba Yonathani ameondoka.
4 Na katikati ya mianya, ambayo Yonathani alitaka kuipitia ili kuifikilia hiyo ngome ya Wafilisti, palikuwa na genge la jabali upande huu, na genge la jabali upande huu; jina la moja liliitwa Bosesi, na jina la pili Sene.
5 Hilo genge moja limesimama upande wa kaskazini, mbele ya Mikmashi, na hilo la pili upande wa kusini, mbele ya Geba.
6 Basi, Yonathani akamwambia yule kijana aliyemchukulia silaha zake, Haya! Na twende tukawavukie ngomeni hao wasiotahiriwa; yamkini Bwana atatutendea kazi; kwa maana hakuna la kumzuia Bwana asiokoe, kwamba ni kwa wengi au kwamba ni kwa wachache.
7 Naye huyo mchukua silaha akamjibu, Fanya yote yaliyomo moyoni mwako; angalia, mimi hapa ni pamoja nawe, moyo wangu ni kama moyo wako.
8 Ndipo Yonathani akasema, Tazama, sisi tutawavukia watu hawa, na kujidhihirisha kwao.
9 Nao wakituambia hivi, Ngojeni, hata sisi tuwafikilie; ndipo tusimame pale pale mahali petu, tusiwapandie.
10 Lakini wakisema hivi, Haya! Ninyi, tupandieni sisi; hapo ndipo tutakapopanda; kwa maana Bwana amewatia mikononi mwetu; na hii itakuwa ndiyo ishara kwetu.
11 Basi, hao wote wawili wakajidhihirisha mbele ya ngome ya Wafilisti, na wale Wafilisti wakasema, Kumbe! Wale Waebrania watoka katika mashimo walimojificha!
12 Nao watu wa ngomeni wakamjibu Yonathani na mchukua silaha zake, wakasema, Haya! Ninyi, pandeni juu hapa tulipo, na sisi tutawaonyesha jambo. Yonathani akamwambia yule aliyezichukua silaha, Haya! Panda nyuma yangu; kwa kuwa Bwana amewatia mikononi mwa Israeli.
13 Basi Yonathani akapanda kwa mikono na miguu yake, na mchukua silaha nyuma yake; na hao watu wakaanguka mbele ya Yonathani; na huyo mchukua silaha zake akawaua nyuma yake.
14 Na uuaji huo wa kwanza walioufanya Yonathani na mchukua silaha zake, ulipata kama watu ishirini, katika nafasi kama nusu ya kiwanja kiwezacho kulimwa katika siku nzima.
15 Kukawa na tetemeko katika marago, na katika mashamba, na katikati ya watu wote; watu wa ngomeni, na watekaji wa nyara, wakatetemeka nao; hata na nchi ikatetemeka pia; basi kulikuwa na tetemeko kubwa mno.
16 Nao wale walinzi wa Sauli huko Gibea ya Benyamini wakaangalia, na tazama, mkutano ule ulikuwa ukitoweka, na watu walikuwa wakienda huko na huko.
17 Ndipo Sauli akawaambia watu waliokuwa pamoja naye, Haya! Hesabuni sasa, mkaone ni nani aliyeondoka kwetu. Nao walipokwisha hesabu, tazama Yonathani na yeye aliyechukua silaha zake hawapo.
18 Basi Sauli akamwambia Ahiya, Lilete hapa sanduku la Mungu. Kwa kuwa hilo sanduku la Mungu wakati huo lilikuwapo pamoja na wana wa Israeli
19 Ikawa Sauli alipokuwa katika kusema na kuhani, hayo makelele katika marago ya Wafilisti yakaendelea na kuzidi; basi Sauli akamwambia kuhani, Rudisha mkono wako.
20 Naye Sauli na watu wote waliokuwapo pamoja naye wakakusanyika, wakaenda vitani; na tazama, huko upanga wa kila mtu ulikuwa juu ya mwenziwe, kukawa fujo tele kabisa.
21 Basi na wale Waebrania waliokuwa pamoja na Wafilisti tangu zamani, wale waliopanda pamoja nao mpaka maragoni toka nchi iliyozunguka; watu hao nao wakageuka kuwa upande wa Waisraeli waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani.
22 Na vile vile watu wote wa Israeli waliokuwa wamejificha katika nchi ya milima milima ya Efraimu, waliposikia ya kwamba Wafilisti wamekimbia, hata hao nao wakawafuatia mbio vitani.
23 Hivyo Bwana akawaokoa Israeli siku ile; na vita vikapita mbele karibu na Beth-aveni. Wakati huo mbele ya wana wa Israeli.
24 Nao watu wa Israeli walisumbuka sana siku ile; lakini Sauli alikuwa amewaapisha watu, akisema, Na alaaniwe mtu awaye yote alaye chakula cho chote hata jioni, nipate kujilipiza kisasi juu ya adui zangu. Basi hakuna mtu miongoni mwa watu aliyeonja chakula.
25 Nao watu wote wakaingia mwituni; na humo mlikuwa na asali juu ya nchi.
26 Na hapo watu walipokwisha kuingia mwituni, tazama, hiyo asali ilikuwa ikidondoka; walakini hakuna mtu hata mmoja aliyetia mkono wake kinywani; kwa sababu hao watu walikuwa wakikiogopa kile kiapo.
27 Ila Yonathani hakusikia, hapo babaye alipowaagiza watu kwa kiapo; basi yeye akainyosha ncha ya fimbo iliyokuwa mkononi mwake, na kuichovya katika sega la asali, kisha akatia mkono wake kinywani; na macho yake yakatiwa nuru.
28 Ndipo mmojawapo wa watu akamjibu, akasema, Baba yako aliwaagiza watu sana kwa kiapo, akisema, Na alaaniwe mtu alaye chakula leo. Na hao watu walikuwa wamepungukiwa na nguvu.
29 Ndipo Yonathani akasema, Babangu ameifadhaisha nchi; tafadhali, angalia jinsi macho yangu yalivyotiwa nuru, kwa sababu nalionja asali hii kidogo.
30 Je! Si zaidi sana, kama watu wangalikula na kushiba leo katika nyara hizi za adui zao walizoziteka? Kwa maana haukuwa uuaji mkuu sasa katikati ya Wafilisti.
31 Nao wakawapiga watu miongoni mwa Wafilisti siku ile kutoka Mikmashi mpaka Ayaloni; na hao watu walikuwa wamepungukiwa sana na nguvu.
32 Basi watu wakazirukia zile nyara, wakatwaa kondoo, na ng'ombe, na ndama, na kuwachinja papo hapo juu ya nchi, nao wale watu walikuwa wakiwala pamoja na damu.
33 Ndipo wakamwambia Sauli, wakisema, Angalia, watu hao wanakosa juu ya Bwana, kwa jinsi wanavyokula pamoja na damu. Naye akasema, Ninyi mmefanya kwa hiana; vingirisheni kwangu leo jiwe kubwa.
34 Kisha Sauli akasema, Haya! Tawanyikeni katikati ya watu mkawaambie, Nileteeni hapa kila mtu ng'ombe wake, na kila mtu kondoo wake, mkawachinje hapa na kula; wala msikose juu ya Bwana, kwa kula pamoja na damu. Nao watu wote wakaleta kila mtu ng'ombe wake pamoja naye usiku ule, nao wakawachinja hapo.
35 Naye Sauli akamjengea Bwana madhabahu; hiyo ndiyo madhabahu ya kwanza aliyomjengea Bwana.
36 Kisha Sauli akasema, Haya! Na tushuke kuwafuata Wafilisti wakati wa usiku, na kuwateka nyara hata mapambazuko, wala tusiwaache hata mmoja wao. Nao wakamjibu, Fanya yo yote uyaonayo kuwa ni mema. Ndipo yule kuhani akasema, Na tumkaribie Mungu hapa.
37 Basi Sauli akataka shauri kwa Mungu, Je! Nishuke ili kuwafuatia Wafilisti? Je! Utawatia mikononi mwa Israeli? Lakini hakumjibu neno lo lote siku ile.
38 Ndipo Sauli akasema, Karibieni hapa, enyi wakuu wote wa watu; mjue na kuona dhambi hii ya leo imekuwa katika kosa gani.
39 Kwa maana, aishivyo Bwana, awaokoaye Israeli, ijapokuwa i katika Yonathani, mwanangu, kufa atakufa. Lakini miongoni mwa watu wote hakuna mtu ye yote aliyemjibu.
40 Ndipo akawaambia Israeli wote, Ninyi mtakuwa upande mmoja, na mimi na mwanangu Yonathani tutakuwa upande wa pili. Basi wakamwambia Sauli, Fanya uonayo kuwa ni mema.
41 Kwa hiyo Sauli akamwambia Bwana, Mungu wa Israeli, [Kwani usimjibu mtumishi wako leo? Ikiwa dhambi i ndani yangu, au ndani yake Yonathani mwanangu, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, utoe Urimu; bali ukisema hivi, Dhambi i katika watu wako Israeli,] utoe Thumimu ,Basi Yonathani na Sauli wakatwaliwa,lakini watu wakapona.
42 Basi Sauli akasema, Sasa piga kati ya mimi na mwanangu Yonathani, [naye awaye yote ambaye Bwana atamtwaa, atakufa. Nao watu wakamwambia Sauli, La! Sivyo hivyo; lakini Sauli akawaweza watu. Nao wakapiga kati ya yeye na mwanawe Yonathani,]
43 Ndipo Sauli akamwambia Yonathani, Niambie ulilolifanya. Basi Yonathani akamwambia, akasema, Ni kweli, mimi nalionja asali kidogo kwa ncha ya fimbo ile iliyokuwa mkononi mwangu; na tazama, imenipasa kufa.
44 Naye Sauli akasema, Mungu anifanyie hivi, na kuzidi; kwa kuwa hakika utakufa, Yonathani.
45 Walakini watu wakamwambia Sauli, Je! Atakufa Yonathani, ambaye ndiye aliyeufanya huo wokovu mkuu katika Israeli? Hasha! Aishivyo Bwana, hautaanguka chini hata unywele mmoja wa kichwa chake; kwa maana ametenda kazi pamoja na Mungu leo. Hivyo hao watu wakamponya Yonathani, asife.
46 Ndipo Sauli akakwea kuacha kuwafuata Wafilisti; nao Wafilisti wakaenda zao kwao.
47 Basi Sauli alipokwisha kuutwaa ufalme juu ya Israeli, alipigana na adui zake zote pande zote, juu ya Moabu, na juu ya wana wa Amoni, na juu ya Edomu, na juu ya wafalme wa Soba, na juu ya Wafilisti; na po pote alipogeukia, akawashinda.
48 Naye akatenda kwa ushujaa, akawapiga Waamaleki, na kuwaokoa Waisraeli katika mikono yao waliowateka nyara.
49 Basi, wana wa Sauli walikuwa ni hawa, Yonathani, na Ishvi, na Malkishua; na majina ya binti zake wawili yalikuwa haya; jina lake wa kwanza aliitwa Merabu, na jina lake mdogo aliitwa Mikali;
50 na jina lake mkewe Sauli aliitwa Ahinoamu, binti Ahimaasi. Tena, jina la jemadari wa jeshi lake aliitwa Abneri, mwana wa Neri, aliyekuwa baba mdogo wa Sauli.
51 Na Kishi, babaye Sauli, na Neri, babaye Abneri, walikuwa wana wa Abieli.
52 Tena, kulikuwa na vita vikali sana juu ya Wafilisti siku zote za Sauli, naye Sauli alipomwona mtu ye yote aliyekuwa hodari, au mtu ye yote aliyekuwa shujaa, humtwaa ili awe pamoja naye.