Mlango 25
1 Akafa Samweli; nao Israeli wote wakakusanyika, wakamwomboleza, wakamzika nyumbani mwake huko Rama.
2 Na huko Maoni kulikuwa na mtu mmoja, ambaye alikuwa na mali yake katika Karmeli; naye yule mtu alikuwa mkuu sana, mwenye kondoo elfu tatu na mbuzi elfu; naye alikuwa akiwakata manyoya kondoo zake huko Karmeli.
3 Na jina la mtu huyo aliitwa Nabali; na jina la mkewe aliitwa Abigaili, na huyo mwanamke alikuwa mwenye akili njema, mzuri wa uso; bali yule mwanamume alikuwa hana adabu, tena mwovu katika matendo yake; naye alikuwa wa mbari ya Kalebu.
4 Basi Daudi akasikia huko nyikani ya kuwa Nabali alikuwa katika kuwakata manyoya kondoo zake.
5 Daudi akatuma vijana kumi, Daudi naye akawaambia hao vijana, Kweeni mwende Karmeli, na kumwendea huyu Nabali ili mnisalimie;
6 na hivi ndivyo mtakavyomwambia huyu aishiye salama, Amani na iwe kwako, na amani nyumbani mwako, na amani kwao wote ulio nao.
7 Nami sasa nimesikia ya kuwa una watu wanaokata manyoya kondoo zako; haya! Wachungaji wako wamekuwa pamoja nasi, wala hatukuwadhuru, wala hawakukosa kitu wakati wote walipokuwako huko Karmeli.
8 Waulize vijana wako, nao watakuambia; basi na wakubaliwe vijana hawa machoni pako; maana tumekujia katika siku ya heri; uwape, nakusihi, cho chote kitakachokujia mkononi, uwape watumwa wako na mwanao Daudi.
9 Basi walipofika vijana wake Daudi, wakamwambia Nabali sawasawa na maneno hayo yote kwa jina la Daudi, kisha wakanyamaza.
10 Naye Nabali akawajibu wale watumishi wa Daudi, akasema, Huyu Daudi ni nani? Na mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumwa wengi wanaomtoroka kila mtu bwana wake!
11 Basi mimi je! Nitwae mkate wangu, na maji yangu, na machinjo yangu niliyowachinjia hao watu wangu wakatao manyoya kondoo zangu, na kuwapa watu ambao siwajui wametoka wapi?
12 Basi vijana wake Daudi wakageuka, wakaenda zao, wakarudi, nao wakaja wakamwambia sawasawa na maneno hayo yote.
13 Kisha Daudi akawaambia watu wake, Haya! Jifungeni kila mtu upanga wake. Nao wakajifunga kila mtu upanga wake; Daudi naye akajifunga upanga wake; nao wakapanda nyuma yake Daudi, wapata kama watu mia nne; na watu mia mbili wakakaa na vyombo vyao.
14 Lakini kijana mmojawapo alimpasha habari Abigaili, mkewe Nabali, kasema, Tazama, Daudi alituma wajumbe kutoka nyikani waje ili kumsalimu bwana wetu, naye akawatukana.
15 Walakini watu hawa walitutendea mema sana, wala hatukupata dhara, wala sisi hatukupotewa na kitu cho chote, wakati wote tulipofuatana nao, tulipokuwako mavueni;
16 watu hao walikuwa boma kwetu usiku na mchana, wakati wote tulipokuwa nao tukiwachunga kondoo.
17 Basi sasa ujue na kufikiri utakayotenda; kwa sababu yamekusudiwa mabaya juu ya bwana wetu, na juu ya nyumba yake yote; kwa kuwa yeye ni mtu asiyefaa kabisa, hata mtu hawezi kusema naye.
18 Ndipo Abigaili akafanya haraka, akatwaa mikate mia mbili, na viriba viwili vya divai, na kondoo watano waliofanyizwa tayari, na vipimo vitano vya bisi, na vishada mia vya zabibu, na mikate ya tini mia mbili; akavipakia vitu hivi juu ya punda.
19 Akawaambia vijana wake, Haya! Tangulieni mbele yangu; angalieni, mimi nawafuata. Ila hakumwambia mumewe, Nabali.
20 Ikawa, alipokuwa amepanda punda wake, na kutelemka penye sitara ya mlima, tazama, Daudi na watu wake walikuwa wakishuka kumkabili; naye akawakuta.
21 Basi Daudi alikuwa amesema, Hakika ni bure nilivyokuwa nikilinda nyikani yote aliyo nayo mtu huyu, asipotewe na kitu cho chote cha mali yake yote; naye amenilipa mabaya badala ya mema.
22 Mungu naye awafanyie hivyo adui za Daudi, na kuzidi, nikimwachia katika wote walio wake hata mtoto mume mmoja, kutakapopambazuka asubuhi.
23 Ndipo hapo Abigaili alipomwona Daudi, alifanya haraka kushuka juu ya punda wake, akamwangukia Daudi kifulifuli, akainama mpaka nchi.
24 Akamwangukia miguuni pake, akasema, Juu yangu, bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako.
25 Nakusihi, bwana wangu, wewe usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani, Nabali; kwa maana kama lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye; jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao; lakini mimi, mjakazi wako, sikuwaona hao vijana wa bwana wangu aliowatuma.
26 Basi sasa, bwana wangu, aishivyo Bwana, na iishivyo nafsi yako, kwa kuwa Bwana amekuzuia usimwage damu, tena usijilipize kisasi mkono wako mwenyewe, basi sasa adui zako, na hao wamtakiao bwana wangu mabaya, wawe kama Nabali.
27 Na sasa zawadi hii, mjakazi wako aliyomletea bwana wangu, na wapewe vijana wamfuatao bwana wangu.
28 Nakuomba ulisamehe kosa lake mjakazi wako, kwa kuwa hakika Bwana atamfanyia bwana wangu nyumba iliyo imara, kwa sababu bwana wangu anavipiga vita vya Bwana; tena uovu hautaonekana ndani yako siku zako zote.
29 Na hata ijapokuwa binadamu angeinuka akuwinde, na kuitafuta nafsi yako, hiyo nafsi ya bwana wangu itafungwa katika furushi ya uhai pamoja na Bwana, Mungu wako; na nafsi za adui zako ndizo atakazozitupa nje, kama kutoka kati ya teo.
30 Tena itakuwa, hapo Bwana atakapokuwa amemtendea bwana wangu sawasawa na mema yote aliyoyanena juu yako, na kukutawaza juu ya Israeli;
31 hili halitakuwa kwazo, wala chukizo la moyoni kwa bwana wangu, ama ya kuwa umemwaga damu bure, ama ya kuwa bwana wangu amejilipiza kisasi mwenyewe; tena hapo Bwana atakapokuwa amemtendea bwana wangu mema, ndipo umkumbuke mjakazi wako.
32 Naye Daudi akamwambia Abigaili, Na ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli, ambaye amekuleta hivi leo kunilaki;
33 na ibarikiwe busara yako, na ubarikiwe wewe, uliyenizuia hivi leo nisimwage damu, wala kujilipiza kisasi kwa mkono wangu mwenyewe.
34 Kwa kuwa ni kweli, aishivyo Bwana, Mungu wa Israeli, aliyenizuia nisikudhuru, kwamba hungefanya haraka kuja kunilaki, hakika huyu Nabali asingaliachiwa hata mtoto mume mmoja, kutakapopambazuka asubuhi.
35 Basi Daudi akapokea mkononi mwake vitu vile alivyomletea; akamwambia, Haya! Kwea kwa amani kwenda nyumbani kwako; tazama, nimeisikiliza sauti yako, nami nimeukubali uso wako.
36 Kisha Abigaili alimjia Nabali; na tazama, alikuwa amefanya karamu nyumbani mwake, kama karamu ya kifalme; na moyo wake huyo Nabali ukafurahiwa ndani yake, kwa maana amelewa kabisa. Kwa sababu hiyo hakumwambia neno, dogo wala kubwa, hata kulipopambazuka.
37 Ikawa asubuhi, divai ilipokuwa imemtoka Nabali, mkewe alimwambia mambo hayo, na moyo wake ukafa ndani yake, akawa kama jiwe.
38 Tena ikawa, yapata siku kumi baadaye, Bwana alimpiga huyo Nabali, hata akafa.
39 Naye aliposikia ya kwamba Nabali amekufa, Daudi alisema, Na ahimidiwe Bwana ambaye amenitetea teto la shutumu langu mkononi mwa Nabali, na kumzuia mtumwa wake asitende maovu; tena uovu wake Nabali Bwana amemrudishia juu ya kichwa chake mwenyewe. Kisha Daudi akatuma watu, akamposa Abigaili ili amwoe.
40 Na hao watumishi wa Daudi walipomjia huyo Abigaili huko Karmeli, walimwambia, wakasema, Daudi ametutuma kwako ili tukutwae uwe mkewe.
41 Naye akainuka na kujiinamisha kifulifuli mpaka nchi, akasema, Tazama, mjakazi wako ni mtumwa wa kuwaosha miguu watumishi wa bwana wangu.
42 Abigaili akafanya haraka, akainuka, akapanda punda, pamoja na vijakazi watano wake waliofuatana naye, akawafuata hao wajumbe wa Daudi, akawa mkewe.
43 Tena Daudi akamwoa Ahinoamu wa Yezreeli; wakawa wote wawili wakeze.
44 Walakini Sauli alikuwa amempa Palti, mwana wa Laishi, aliyekuwa mtu wa Galimu, Mikali binti yake, aliyekuwa mkewe Daudi.