Mlango 13
1 Sauli alikuwa na umri wa miaka kadha wa kadha hapo alipoanza kutawala;naye akatawala miaka kadha wa kadha juu ya Israeli.
2 Naye Sauli alijichagulia watu elfu tatu wa Israeli; ambao katika hao, elfu mbili walikuwa pamoja na Sauli katika Mikmashi, na katika mlima wa Betheli na elfu moja pamoja na Yonathani katika Gibea ya Benyamini; nao wale watu waliosalia akawaruhusu waende kila mtu hemani kwake.
3 Yonathani akaipiga hiyo ngome ya Wafilisti, iliyokuwako huko Gibea, nao Wafilisti wakapata habari. Naye Sauli akapiga tarumbeta katika nchi yote, huku akisema, Na wasikie Waebrania.
4 Waisraeli wote wakasikia habari ya kwamba Sauli ameipiga hiyo ngome ya Wafilisti, na ya kwamba Waisraeli wamepata kuwa makuruhi kwa Wafilisti. Basi hao watu wakakusanyika pamoja kumfuata Sauli huko Gilgali.
5 Nao Wafilisti wakakusanyana ili wapigane na Waisraeli, magari thelathini elfu, na wapanda farasi sita elfu, na watu kama mchanga ulio ufuoni mwa bahari kwa wingi wao; wakapanda juu, wakapiga kambi yao katika Mikmashi, upande wa mashariki wa Beth-aveni.
6 Hata Waisraeli walipoona ya kuwa wa katika dhiki, (maana watu walifadhaishwa), ndipo hao watu wakajificha katika mapango, na katika vichaka, na katika miamba, na katika mashimo, na katika mabirika.
7 Hata baadhi ya Waebrania walivuka Yordani, wakaingia nchi ya Gadi na Gileadi; lakini Sauli alikuwa akaliko huko Gilgali, nao watu wote wakamfuata wakitetemeka.
8 Akangoja siku saba, kwa kadiri ya muhula uliowekwa na Samweli lakini Samweli hakuja Gilgali; na hao watu wakatawanyika mbali naye.
9 Sauli akasema, Nileteeni hapa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani. Akaitoa sadaka ya kuteketezwa.
10 Hata mara alipokwisha kuitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, kumbe! Samweli akatokea. Naye Sauli akatoka kwenda kumlaki na kumsalimu.
11 Samweli akasema, Umefanya nini? Naye Sauli akasema, Ni kwa sababu naliona ya kuwa watu wanatawanyika mbali nami, na wewe hukuja siku zile zilizonenwa; nao Wafilisti wamekusanyika pamoja huko Mikmashi;
12 basi nikasema, Wafilisti watanishukia sasa mpaka Gilgali, kabla sijaomba fadhili za Bwana; kwa hiyo nalijishurutisha, nikatoa sadaka ya kuteketezwa.
13 Naye Samweli akamwambia Sauli, Umefanya upumbavu; hukuishika amri ya Bwana, Mungu wako, aliyokuamuru; kwa maana Bwana angaliufanya ufalme wako kuwa imara juu ya Israeli milele.
14 Lakini sasa ufalme wako hautadumu; Bwana amejitafutia mtu aupendezaye moyo wake, naye Bwana amemwamuru yeye kuwa mkuu juu ya watu wake, kwa sababu wewe hukulishika neno lile Bwana alilokuamuru.
15 Basi Samweli akaondoka, akapanda kutoka Gilgali mpaka Gibea ya Benyamini. Naye Sauli akawahesabu watu waliokuwapo pamoja naye, wapata kama mia sita.
16 Naye Sauli, na mwanawe Yonathani, na watu waliokuwapo pamoja nao, wakakaa huko Geba ya Benyamini; lakini Wafilisti wakatua katika Mikmashi.
17 Nao watekaji wa nyara wakatoka katika marago ya hao Wafilisti, vikosi vitatu; kikosi kimoja kikageukia njia iendayo Ofra, mpaka nchi ya Shuali;
18 na kikosi kingine kikageukia njia iendayo Beth-horoni; na kikosi kingine kikageukia njia ya mpakani ielekeayo bonde la Seboimu upande wa nyika.
19 Basi, hakuonekana mhunzi ye yote katika nchi yote ya Israeli; kwa kuwa Wafilisti walisema, Waebrania wasije wakajifanyizia panga au mikuki;
20 lakini Waisraeli wote hushuka kwa Wafilisti, ili kunoa kila mtu jembe lake, na mundu wake, na shoka lake, na sululu yake;
21 ila walikuwa na tupa za kunolea sululu, na miundu, na mauma, na mashoka; na kwa kuinoa michokoo.
22 Hivyo ikawa, siku ya vita, haukuonekana mkononi mwa mtu ye yote, miongoni mwa watu waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani, upanga wala mkuki; isipokuwa Sauli mwenyewe na mwanawe Yonathani walikuwa navyo.
23 Na jeshi la Wafilisti wakatoka hata mwanya wa Mikmashi.