Mlango 26
1 Kama theluji wakati wa joto, na mvua wakati wa mavuno; Kadhalika heshima haimpasi mpumbavu.
2 Kama shomoro katika kutanga-tanga kwake, Na kama mbayuwayu katika kuruka kwake; Kadhalika laana isiyo na sababu haimpigi mtu.
3 Mjeledi kwa farasi, lijamu kwa punda, Na fimbo kwa mgongo wa mpumbavu.
4 Usimjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake; Usije ukafanana naye.
5 Umjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake; Asije akawa mwenye hekima machoni pake.
6 Apelekaye ujumbe kwa mkono wa mpumbavu Hujikata miguu, na kunywa hasara.
7 Miguu yake achechemeaye huwa dhaifu; Kadhalika mithali katika kinywa cha mpumbavu.
8 Kama mfuko wa vito katika chungu ya mawe; Kadhalika mtu amheshimuye mpumbavu.
9 Kama mwiba uingiao katika mkono wa mlevi; Kadhalika mithali katika kinywa cha mpumbavu.
10 Fundi stadi hufanyiza vitu vyote; Bali amwajiriye mpumbavu ni kama awaajiriye watu wapitao.
11 Kama vile mbwa arudiavyo matapiko yake; Kadhalika mpumbavu afanya upumbavu tena.
12 Je! Wamwona mtu mwenye hekima machoni pake mwenyewe? Afadhali kumtumaini mpumbavu kuliko yeye.
13 Mtu mvivu husema, Simba yuko njiani, Simba yuko katika njia kuu.
14 Kama vile mlango ugeukavyo katika bawaba zake; Kadhalika mtu mvivu katika kitanda chake.
15 Mtu mvivu hutia mkono wake sahanini; Kwamchosha kuupeleka tena kinywani pake.
16 Mtu mvivu ni mwenye hekima machoni pake, Kuliko watu saba wawezao kutoa sababu.
17 Mtu apitaye na kujisumbua kwa ugomvi usio wake; Ni kama mtu ashikaye mbwa kwa masikio yake.
18 Kama mtu mwenye wazimu atupaye mienge, Na mishale, na mauti;
19 Ndivyo alivyo amdanganyaye mwenzake, Na kusema, Je! Sikufanya mzaha tu?
20 Moto hufa kwa kukosa kuni; Na bila mchongezi fitina hukoma.
21 Kama makaa juu ya makaa yanayowaka, Na kama kuni juu ya moto; Ndivyo mtu mgomvi achocheavyo uadui.
22 Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo. Nayo hushukia pande za ndani za tumbo.
23 Midomo ijipendekezayo pamoja na moyo mbaya Ni kama kigae kilichofunikizwa taka za fedha.
24 Achukiaye huficha chuki kwa midomo yake; Naye huweka akiba ya hila moyoni mwake.
25 Anenapo maneno mazuri usimsadiki; Kwa maana ana machukizo saba moyoni mwake.
26 Ingawa chuki hufunikizwa kwa hila; Uovu wake utadhihirika mbele ya kusanyiko.
27 Achimbaye shimo atatumbukia mwenyewe; Naye abingirishaye jiwe litamrudia.
28 Ulimi unenao uongo huwachukia wale uliowajeruhi; Na kinywa cha kujipendekeza hutenda uharibifu.