Mlango 23
1 Utakapoketi kwa chakula pamoja na mtawala, Mwangalie sana yeye aliye mbele yako.
2 Tena ujitie kisu kooni, Kama ukiwa mlafi.
3 Usivitamani vyakula vyake vya anasa; Kwa maana ni vyakula vya hila.
4 Usijitaabishe ili kupata utajiri; Acha kuzitegemea akili zako mwenyewe.
5 Je! Utavikazia macho vile ambavyo si kitu? Maana bila shaka mali hujifanyia mabawa, Kama tai arukaye mbinguni.
6 Usile mkate wa mtu mwenye husuda; Wala usivitamani vyakula vyake vya anasa;
7 Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo. Akuambia, Haya, kula, kunywa; Lakini moyo wake hauwi pamoja nawe.
8 Tonge lile ulilokula utalitapika, Na maneno yako matamu yatakupotea.
9 Usiseme masikioni mwa mpumbavu; Maana atadharau hekima ya maneno yako.
10 Usiiondoe alama ya mpaka wa zamani; Wala usiingie katika mashamba ya yatima;
11 Kwa sababu mkombozi wao ana nguvu; Atawatetea juu yako.
12 Elekeza moyo wako kusikiliza mafundisho; Tega masikio yako kusikia maneno ya maarifa.
13 Usimnyime mtoto wako mapigo; Maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa.
14 Utampiga kwa fimbo, Na kumwokoa nafsi yake na Kuzimu.
15 Mwanangu, kama moyo wako una hekima, Moyo wangu utafurahi, naam, moyo wangu;
16 Naam, viuno vyangu vitafurahi, Midomo yako inenapo maneno mema.
17 Moyo wako usiwahusudu wenye dhambi; Bali mche Bwana mchana kutwa;
18 Maana bila shaka iko thawabu; Na tumaini lako halitabatilika.
19 Sikia, mwanangu, uwe na hekima, Na kuuongoza moyo wako katika njia njema.
20 Usiwe miongoni mwao wanywao mvinyo; Miongoni mwao walao nyama kwa pupa.
21 Kwa maana mlevi na mlafi huingia umaskini, Na utepetevu humvika mtu nguo mbovu.
22 Msikilize baba yako aliyekuzaa, Wala usimdharau mama yako akiwa mzee.
23 Inunue kweli, wala usiiuze; Naam, hekima, na mafundisho, na ufahamu.
24 Baba yake mwenye haki atashangilia; Naye amzaaye mtoto mwenye hekima atamfurahia.
25 Na wafurahi baba yako na mama yako; Na afurahi aliyekuzaa.
26 Mwanangu, nipe moyo wako; Macho yako yapendezwe na njia zangu.
27 Kwa maana kahaba ni shimo refu; Na malaya ni rima jembamba.
28 Naam, huotea kama mnyang'anyi; Huwaongeza wenye hila katika wanadamu.
29 Ni nani apigaye, Yowe? Ni nani aliaye, Ole? Ni nani mwenye ugomvi? Ni nani mwenye mguno? Ni nani aliye na jeraha zisizo na sababu? Ni nani aliye na macho mekundu?
30 Ni wale wakaao sana kwenye mvinyo; Waendao kutafuta divai iliyochanganyika.
31 Usiitazame mvinyo iwapo ni nyekundu; Iitiapo bilauri rangi yake, ishukapo taratibu;
32 Mwisho wake huuma kama nyoka; Huchoma kama fira.
33 Macho yako yataona mambo mageni; Na moyo wako utatoa yaliyopotoka.
34 Naam, utakuwa kama alalaye katikati ya bahari; Au kama yeye asinziaye juu ya mlingoti.
35 Utasema, Wamenichapa wala sikuumia; Wamenipiga wala sina habari; Nitaamka lini, nitazidi kuitafuta tena.