Mlango 58
1 Ni kweli, enyi wakuu, mnanena haki? Enyi wanadamu, mnahukumu kwa adili?
2 Sivyo! Mioyoni mwenu mnatenda maovu; Katika nchi mnapima udhalimu wa mikono yenu.
3 Wasio haki wamejitenga tangu kuzaliwa kwao; Tangu tumboni wamepotea, wakisema uongo.
4 Sumu yao, mfano wake ni sumu ya nyoka; Mfano wao ni fira kiziwi azibaye sikio lake.
5 Asiyeisikiliza sauti ya waganga, Ijapo wanafanya uganga kwa ustadi.
6 Ee Mungu, uyavunje meno yao vinywani mwao; Ee Bwana, uyavunje magego ya wana-simba.
7 Na watoweke kama maji yapitayo kwa kasi; Akiielekeza mishale yake, iwe imetiwa ubutu.
8 Kama konokono ayeyukaye na kutoweka, Kama mimba iliyoharibika, isiyoliona jua,
9 Kabla ya masufuria yenu kupata moto wa miiba, Ataipeperusha kama chamchela, Iliyo mibichi na iliyo moto.
10 Mwenye haki atafurahi akionapo kisasi; Ataiosha miguu yake katika damu ya wasio haki.
11 Na mwanadamu atasema, Hakika iko thawabu yake mwenye haki. Hakika yuko Mungu Anayehukumu katika dunia.