Mlango 78
1 Enyi watu wangu, sikilizeni sheria yangu, Tegeni masikio kwa maneno ya kinywa changu.
2 Na nifunue kinywa changu kwa mithali, Niyatamke mafumbo ya kale.
3 Mambo tuliyoyasikia na kuyafahamu, Ambayo baba zetu walituambia.
4 Hayo hatutawaficha wana wao, Huku tukiwaambia kizazi kingine, Sifa za Bwana, na nguvu zake, Na mambo yake ya ajabu aliyoyafanya.
5 Maana alikaza ushuhuda katika Yakobo, Na sheria aliiweka katika Israeli. Aliyowaamuru baba zetu Wawajulishe wana wao,
6 Ili kizazi kingine wawe na habari, Ndio hao wana watakaozaliwa. Wasimame na kuwaambia wana wao
7 Wamwekee Mungu tumaini lao. Wala wasiyasahau matendo ya Mungu, Bali wazishike amri zake.
8 Naam, wasiwe kama baba zao, Kizazi cha ukaidi na uasi. Kizazi kisichojitengeneza moyo, Wala roho yake haikuwa amini kwa Mungu.
9 Wale Waefraimu, wenye silaha, wapiga upinde, Walirudi nyuma siku ya vita.
10 Hawakulishika agano la Mungu; Wakakataa kuenenda katika sheria yake;
11 Wakayasahau matendo yake, Na mambo yake ya ajabu aliyowaonyesha.
12 Mbele ya baba zao alifanya mambo ya ajabu, Katika nchi ya Misri, konde la Soani.
13 Aliipasua bahari akawavusha; Aliyasimamisha maji mfano wa chungu.
14 Akawaongoza kwa wingu mchana, Na usiku kucha kwa nuru ya moto.
15 Akapasua miamba jangwani; Akawanywesha maji mengi kama maji ya vilindi.
16 Akatokeza na vijito gengeni, Akatelemsha maji kama mito.
17 Lakini wakazidi kumtenda dhambi, Walipomwasi Aliye juu katika nchi ya kiu.
18 Wakamjaribu Mungu mioyoni mwao Kwa kutaka chakula kwa tamaa zao.
19 Naam, walimwamba Mungu, wakasema, Je! Mungu aweza kuandika meza jangwani?
20 Tazama, aliupiga mwamba; Maji yakabubujika, ikafurika mito. Pia aweza kutupa chakula? Atawaandalia watu wake nyama?
21 Hivyo Bwana aliposikia akaghadhibika; Moto ukawashwa juu ya Yakobo, Hasira nayo ikapanda juu ya Israeli.
22 Kwa kuwa hawakumwamini Mungu, Wala hawakuutumainia wokovu wake.
23 Lakini aliyaamuru mawingu juu; Akaifungua milango ya mbinguni;
24 Akawanyeshea mana ili wale; Akawapa nafaka ya mbinguni.
25 Mwanadamu akala chakula cha mashujaa; Aliwapelekea chakula cha kuwashibisha.
26 Aliuelekeza upepo wa mashariki mbinguni; Akaiongoza kusi kwa uweza wake.
27 Akawanyeshea nyama kama mavumbi, Na ndege wenye mbawa, Kama mchanga wa bahari.
28 Akawaangusha kati ya matuo yao, Pande zote za maskani zao.
29 Wakala wakashiba sana; Maana aliwaletea walivyovitamani;
30 Hawakuachana na matakwa yao. Ila chakula chao kikali ki vinywani mwao
31 Hasira ya Mungu ikapanda juu yao, Akawaua waliokuwa wanono; Akawaangusha chini vijana wa Israeli.
32 Pamoja na hayo wakazidi kutenda dhambi, Wala hawakuyaamini matendo yake ya ajabu.
33 Kwa hiyo akazikomesha siku zao kama pumzi, Na miaka yao kwa hofu ya kuwasitusha.
34 Alipowaua ndipo walipokuwa wakimtafuta; Wakarudi wakamtaka Mungu kwa bidii.
35 Wakakumbuka kuwa Mungu ni mwamba wao, Na Mungu Aliye juu ni mkombozi wao.
36 Lakini walimdanganya kwa vinywa vyao, Wakamwambia uongo kwa ndimi zao.
37 Kwa maana mioyo yao haikuwa thabiti kwake, Wala hawakuwa waaminifu katika agano lake.
38 Lakini Yeye, kwa kuwa anayo rehema, Husamehe uovu wala haangamizi. Mara nyingi huipishia mbali ghadhabu yake, Wala haiwashi hasira yake yote.
39 Akakumbuka ya kuwa wao ni kiwiliwili, Upepo upitao wala haurudi.
40 Walimwasi jangwani mara ngapi? Na kumhuzunisha nyikani!
41 Wakarudi nyuma wakamjaribu Mungu; Wakampa mpaka Mtakatifu wa Israeli.
42 Hawakuukumbuka mkono wake, Wala siku ile alipowakomboa na mtesi.
43 Alivyoziweka ishara zake katika Misri, Na miujiza yake katika konde la Soani.
44 Aligeuza damu mito yao, Na vijito wasipate kunywa.
45 Aliwapelekea mainzi wakawala, Na vyura wakawaharibu.
46 Akawapa tunutu mazao yao, Na nzige kazi yao.
47 Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe, Na mikuyu yao kwa mawe ya barafu.
48 Akaacha ng'ombe zao wapigwe kwa mvua ya mawe, Na makundi yao kwa umeme.
49 Akawapelekea ukali wa hasira yake, Ghadhabu, na uchungu, na taabu, Kundi la malaika waletao mabaya.
50 Akiifanyizia njia hasira yake; Wala hakuziepusha roho zao na mauti, Bali aliiachia tauni uhai wao;
51 Akampiga kila mzaliwa wa kwanza wa Misri, Malimbuko ya nguvu katika hema za Hamu.
52 Bali aliwaongoza watu wake kama kondoo, Akawachunga kama kundi jangwani.
53 Hao akawachukua salama wala hawakuogopa, Bali bahari iliwafunikiza adui zao.
54 Akawapeleka hadi mpaka wake mtakatifu, Mlima alioununua kwa mkono wake wa kuume.
55 Akawafukuza mataifa mbele yao, Akawapimia urithi kwa kamba, Na kuwakalisha kabila za Israeli katika hema zao.
56 Lakini walimjaribu Mungu Aliye juu, wakamwasi, Wala hawakuzishika shuhuda zake.
57 Bali walirudi nyuma, wakahaini kama baba zao; Wakaepea kama upinde usiofaa.
58 Wakamkasirisha kwa mahali pao pa juu, Wakamtia wivu kwa sanamu zao.
59 Mungu akasikia, akaghadhibika, Akamkataa Israeli kabisa.
60 Akaiacha maskani ya Shilo, Hema aliyoiweka katikati ya wanadamu;
61 Akaziacha nguvu zake kutekwa, Na fahari yake mkononi mwa mtesi.
62 Akawatoa watu wake wapigwe kwa upanga; Akaughadhibikia urithi wake.
63 Moto ukawala vijana wao, Wanawali wao hawakuimbiwa nyimbo za arusi,
64 Makuhani wao walianguka kwa upanga, Wala wajane wao hawakuomboleza.
65 Ndipo Bwana alipoamka kama aliyelala usingizi, Kama shujaa apigaye kelele sababu ya mvinyo;
66 Akawapiga watesi wake akawarudisha nyuma, Akawatia aibu ya milele.
67 Ila akaikataa hema ya Yusufu; Wala hakuichagua kabila ya Efraimu.
68 Bali aliichagua kabila ya Yuda, Mlima Sayuni alioupenda.
69 Akajenga patakatifu pake kama vilele, Kama dunia aliyoiweka imara milele.
70 Akamchagua Daudi, mtumishi wake, Akamwondoa katika mazizi ya kondoo.
71 Nyuma ya kondoo wanyonyeshao alimwondoa, Awachunge Yakobo watu wake, na Israeli urithi wake.
72 Akawalisha kwa ukamilifu wa moyo wake, Na kuwaongoza kwa busara ya mikono yake.