Mlango 7
1 Basi Sulemani alipokwisha maombi hayo, moto ukashuka kutoka mbinguni, ukateketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; utukufu wa Bwana ukaijaza nyumba.
2 Wala makuhani hawakuweza kuingia nyumbani mwa Bwana, kwa kuwa utukufu wa Bwana umeijaza nyumba ya Bwana.
3 Wakatazama wana wa Israeli wote, uliposhuka ule moto, utukufu wa Bwana ulipokuwapo juu ya nyumba; wakasujudu kifulifuli hata nchi sakafuni, wakaabudu, wakamshukuru Bwana, wakisema, Kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za milele.
4 Ndipo mfalme na watu wote wakatoa dhabihu mbele za Bwana.
5 Mfalme Sulemani akatoa sadaka ya ng'ombe ishirini na mbili elfu, na kondoo mia na ishirini elfu. Ndivyo mfalme na watu wote walivyoifanya wakfu nyumba ya Mungu.
6 Wakasimama makuhani sawasawa na malinzi yao; Walawi nao pamoja na vinanda vya Bwana, alivyovifanya Daudi mfalme, ili kumshukuru Bwana, kwa maana fadhili zake ni za milele, hapo aliposifu Daudi kwa mikono yao; nao makuhani wakapiga panda mbele yao; nao Israeli wote wakasimama.
7 Tena Sulemani akaitakasa behewa katikati, iliyokuwa mbele ya nyumba ya Bwana; kwa kuwa hapo ndipo alipotoa sadaka za kuteketezwa, na mafuta ya sadaka za amani; kwa sababu ile madhabahu ya shaba aliyoifanya Sulemani haikutosha kuzipokea sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na mafuta.
8 Basi, wakati ule Sulemani akafanya sikukuu, na Israeli wote pamoja naye, kusanyiko kubwa sana, toka maingilio ya Hamathi mpaka kijito cha Misri, muda wa siku saba.
9 Hata siku ya nane wakaita kusanyiko la makini; kwa maana walishika kuitakasa madhabahu siku saba, na sikukuu siku saba.
10 Akawaruhusu watu waende hemani kwao siku ya ishirini na tatu, ya mwezi wa saba, wakifurahi na kuchangamka mioyoni kwa wema wote Bwana aliomfanyia Daudi, na Sulemani, na Israeli watu wake.
11 Hivyo Sulemani akaimaliza nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme; na yote yaliyomwingia Sulemani moyoni ayafanye nyumbani mwa Bwana, na nyumbani mwake mwenyewe, akayafanikisha.
12 Bwana akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu.
13 Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni;
14 ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.
15 Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.
16 Maana sasa nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, ili kwamba jina langu lipate kuwako huko milele; yatakuwako na macho yangu, na moyo wangu daima.
17 Nawe, ukienda mbele yangu kama alivyokwenda Daudi baba yako, ufanye sawasawa na yote niliyokuamuru, na kuzishika sheria zangu na hukumu zangu;
18 ndipo nitakithibitisha kiti cha enzi cha ufalme wako, kama nilivyoagana na Daudi baba yako, nikisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kutawala katika Israeli.
19 Lakini mkigeuka, na kuziacha sheria zangu na amri zangu nilizoweka mbele yenu, mkienda, na kuitumikia miungu mingine, na kuiabudu;
20 ndipo nitawang'oa katika nchi yangu niliyowapa; na nyumba hii niliyoitakasa kwa jina langu, nitaiondosha itoke mbele zangu, nami nitaifanya kuwa mithali na tukano katikati ya watu wote.
21 Na nyumba hii, iliyo juu, kila apitaye ataona ushangao, atasema, Mbona Bwana ameitendea hivi nchi hii, na nyumba hii?
22 Nao watajibu, Kwa sababu walimwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine, wakaiabudu, na kuitumikia; kwa hiyo ameyaleta mabaya haya yote juu yao.