Mlango 11
1 Hata Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akakusanya nyumba ya Yuda na Benyamini, watu wateule mia na themanini elfu waliokuwa hodari, watu wa vita, ili wapigane juu ya Israeli, ili wamrudishie Rehoboamu huo ufalme.
2 Lakini neno la Bwana likamjia Shemaya mtu wa Mungu, kusema,
3 Mwambie Rehoboamu mwana wa Sulemani, mfalme wa Yuda, uwaambie na Israeli wote waliomo Yuda na Benyamini, ukisema,
4 Bwana asema hivi, Hamtapanda wala kupigana na ndugu zenu; rudini kila mtu nyumbani kwake; kwa kuwa jambo hili limetoka kwangu. Basi, wakayasikiliza maneno ya Bwana, wakarudi katika kumwendea Yeroboamu.
5 Naye Rehoboamu akakaa Yerusalemu, akajenga miji yenye ngome katika Yuda.
6 Akajenga na Bethlehemu, na Etamu, na Tekoa,
7 na Bethsuri, na Soko, na Adulamu,
8 na Gathi, na Maresha, na Zifu,
9 na Adoraimu, na Lakishi, na Azeka,
10 na Sora, na Aiyaloni, na Hebroni, iliyoko katika Yuda na Benyamini, miji yenye maboma.
11 Akazifanya imara hizo ngome, akaweka majemadari humo, na akiba ya vyakula, na mafuta, na mvinyo.
12 Na ndani ya miji yote mmoja mmoja aliweka ngao na mikuki, akaifanya kuwa na nguvu nyingi mno. Yuda na Benyamini ikawa milki yake.
13 Wakamwendea makuhani na Walawi waliokuwa katika Israeli yote, kutoka mpaka wao wote.
14 Kwani Walawi wakaacha malisho yao, na milki yao, wakaja Yuda na Yerusalemu; kwa sababu Yeroboamu na wanawe waliwatupa, ili wasimfanyie Bwana ukuhani;
15 naye akajiwekea makuhani wa mahali pa juu, na wa wale majini, na wa zile ndama alizozifanya.
16 Na kutoka katika kabila zote za Israeli, wakaandamwa na hao waliojikaza nia kumtafuta Bwana, Mungu wa Israeli, wakaja Yerusalemu, ili wamtolee dhabihu Bwana, Mungu wa baba zao.
17 Hivyo wakaufanya imara kwa miaka mitatu ufalme wa Yuda, na kumtia nguvu Rehoboamu mwana wa Sulemani; kwa maana muda wa miaka mitatu wakaiendea njia ya Daudi na Sulemani.
18 Rehoboamu akaoa mke, Mahalathi binti Yerimothi mwana wa Daudi, na wa Abihaili binti Eliabu, mwana wa Yese;
19 akamzalia wana, Yeushi, na Shemaria, na Zahamu.
20 Kisha baada yake akamwoa Maaka, binti Absalomu; na yeye akamzalia Abiya, na Atai, na Ziza, na Shelomithi.
21 Rehoboamu akampenda Maaka binti Absalomu kuliko wakeze wote na masuria yake; (maana alioa wake kumi na wanane, na masuria sitini, akazaa wana ishirini na wanane na binti sitini).
22 Rehoboamu akamsimamisha Abiya, mwana wa Maaka, kuwa mkuu, mtawala kati ya nduguze, kwa kuwa aliazimia kumtawaza awe mfalme.
23 Akafanya kwa akili, akawatawanya wanawe wote kati ya nchi zote za Yuda na Benyamini, katika kila mji wenye boma; akawapa vyakula tele. Akawatafutia wake wengi.