Mlango 30
1 Hezekia akatuma wajumbe kwa Israeli wote na Yuda pia; akawaandikia nyaraka Efraimu na Manase, waje nyumbani kwa Bwana Yerusalemu, ili wamfanyie pasaka Bwana, Mungu wa Israeli.
2 Kwa maana mfalme na wakuu wake, na kusanyiko lote katika Yerusalemu walifanya shauri kufanya pasaka mwezi wa pili.
3 Kwa sababu hawakuweza kuifanya wakati ule, kwa kuwa makuhani walikuwa hawajajitakasa wa kutosha, wala watu hawajakusanyika huko Yerusalemu.
4 Likawa neno jema machoni pa mfalme, na kusanyiko lote.
5 Basi wakafanya amri kupiga mbiu kati ya Israeli yote, toka Beer-sheba mpaka Dani, ya kwamba watu waje wamfanyie pasaka Bwana, Mungu wa Israeli, huko Yerusalemu; maana tangu siku nyingi hawakuifanya kama vile ilivyoandikwa.
6 Wakaenda matarishi wenye nyaraka za mfalme na wakuu wake, kati ya Israeli yote na Yuda, na kwa amri ya mfalme, kusema, Enyi wana wa Israeli, mrudieni Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, apate kuwarudia waliosalia wenu waliookoka mikononi mwa wafalme wa Ashuru.
7 Wala msiwe kama baba zenu, na kama ndugu zenu, waliomwasi Bwana, Mungu wa baba zao, hata akawatoa kuwa ushangao, kama mwonavyo.
8 Msiwe sasa wenye shingo ngumu kama baba zenu; lakini mjitoe kwa Bwana, mkaingie katika patakatifu pake, alipopatakasa milele, mkamtumikie Bwana, Mungu wenu, hasira yake kali iwageukie mbali.
9 Kwa kuwa mkimrudia Bwana, ndugu zenu na watoto wenu watahurumiwa machoni pa hao waliowachukua mateka, nao watairudia nchi hii; kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, ndiye mwenye neema, na mwenye rehema, wala hatawageuzia mbali uso wake, mkimrudia.
10 Basi matarishi wakapita mji kwa mji kati ya nchi ya Efraimu na Manase, hata kufika Zabuloni; lakini waliwacheka-cheka, na kuwadhihaki.
11 Ila watu wengine wa Asheri, na wa Manase, na wa Zabuloni walijinyenyekeza, wakaja Yerusalemu.
12 Tena katika Yuda mkono wa Mungu ulikuwa ukiwapa moyo mmoja, waitimize amri ya mfalme na wakuu kwa neno la Bwana.
13 Basi wakakusanyika Yerusalemu watu wengi ili kuifanya sikukuu ya mikate isiyochachwa katika mwezi wa pili, kusanyiko kuu sana.
14 Wakainuka, wakaziondoa madhabahu zilizokuwamo Yerusalemu, nazo madhabahu za kufukizia wakaziondoa, wakazitupa katika kijito Kidroni.
15 Kisha wakaichinja pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili, nao makuhani na Walawi wakatahayarika, wakajitakasa, wakaleta sadaka za kuteketezwa nyumbani mwa Bwana.
16 Wakasimama mahali pao kwa taratibu yao, sawasawa na torati ya Musa, mtu wa Mungu; nao makuhani wakainyunyiza damu, waliyoipokea mikononi mwa Walawi.
17 Kwa maana kulikuwa na wengi katika kusanyiko ambao hawajajitakasa; kwa hiyo Walawi wakamchinjia pasaka, kila mtu asiyekuwa safi, ili kuwatakasa kwa Bwana.
18 Kwani wingi wa watu, naam, wengi wa Efraimu, na wa Manase, na wa Isakari, na wa Zabuloni, hawakujisafisha, lakini wakala pasaka, ila si kama ilivyoandikwa. Naye Hezekia alikuwa amewaombea, akisema, Bwana mwema na amsamehe kila mtu,
19 aukazaye moyo wake kumtafuta Mungu, Bwana, Mungu wa babaze, hata ikiwa si kwa utakaso wa patakatifu.
20 Bwana akamsikia Hezekia, akawaponya watu.
21 Nao wana wa Israeli waliohudhuria Yerusalemu wakafanya sikukuu ya mikate isiyochachwa siku saba kwa furaha kubwa; Walawi na makuhani wakamsifu Bwana siku kwa siku, wakimwimbia Bwana kwa vinanda vyenye sauti kuu.
22 Hezekia akawafurahisha mioyo Walawi wote waliokuwa wastadi wa kumtumikia Bwana. Basi muda wa siku saba wakala sikukuu, wakitoa dhabihu za sadaka za amani, na kumtolea shukrani Bwana, Mungu wa baba zao.
23 Na kusanyiko lote wakafanya shauri kufanya sikukuu siku saba nyingine; wakafanya sikukuu siku saba nyingine kwa furaha.
24 Maana Hezekia, mfalme wa Yuda, aliwatolea kusanyiko matoleo ya ng'ombe elfu, na kondoo elfu saba; na wakuu wakawatolea kusanyiko ng'ombe elfu, na kondoo elfu kumi; tena wakajitakasa makuhani wengi sana.
25 Na kusanyiko lote la Yuda, pamoja na makuhani na Walawi, na kusanyiko lote waliotoka Israeli, na wageni waliotoka katika nchi ya Israeli, nao waliokaa Yuda, wakafurahi.
26 Ikawa furaha kuu katika Yerusalemu; kwa sababu tangu siku za Sulemani mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli, hayajakuwako mambo kama hayo huko Yerusalemu.
27 Ndipo wakasimama makuhani Walawi, wakawabariki watu; ikasikiwa sauti yao, sala yao ikafika hata makao yake matakatifu, yaani, mbinguni.