Mlango 9
1 Hekima umeijenga nyumba yake, Amezichonga nguzo zake saba;
2 Amechinja nyama zake, umechanganya divai yake, Ameiandalia meza yake pia.
3 Amewatuma wajakazi wake, analia, Mahali pa mjini palipoinuka sana,
4 Kila aliye mjinga na aingie humu. Tena amwambia mtu aliyepungukiwa na akili,
5 Njoo ule mkate wangu, Ukanywe divai niliyoichanganya.
6 Enyi wajinga, acheni ujinga, mkaishi, Mkaende katika njia ya ufahamu.
7 Amkemeaye mwenye dharau hujipatia fedheha; Amkaripiaye mtu mbaya hujipatia aibu.
8 Usimkaripie mwenye dharau, asije akakuchukia; Mkaripie mwenye hekima, naye atakupenda.
9 Mwelimishe mwenye hekima, naye atazidi kuwa na hekima; Mfundishe mwenye haki, naye atazidi kuwa na elimu;
10 Kumcha Bwana ni mwanzo wa hekima; Na kumjua Mtakatifu ni ufahamu.
11 Maana, kwa msaada wangu siku zako zitazidishwa; Na miaka ya maisha yako itaongezwa.
12 Kama una hekima, una hekima kwa nafsi yako; Na kama una dharau, utaichukua peke yako.
13 Mwanamke mpumbavu hupiga kelele, Ni mjinga, hajui kitu.
14 Hukaa mlangoni pa nyumba yake, Juu ya kiti mahali pa mjini palipoinuka,
15 Apate kuwaita wapitao njiani, Waendao moja kwa moja katika njia zao.
16 Kila aliye mjinga na aingie humu. Tena amwambia mtu aliyepungukiwa na akili,
17 Maji yaliyoibiwa ni matamu, Na mkate ulioliwa kwa siri hupendeza.
18 Lakini huyo hajui ya kuwa wafu wamo humo; Ya kuwa wageni wake wamo chini kuzimuni.