Mlango 25
1 Hizi nazo ni mithali za Sulemani, ambazo watu wa Hezekia, mfalme wa Yuda, walizinakili.
2 Ni utukufu wa Mungu kuficha jambo; Bali ni utukufu wa mfalme kuchunguza jambo.
3 Mbingu huenda juu sana, na nchi huenda chini; Lakini mioyo ya wafalme haichunguziki.
4 Ondoa takataka katika fedha, Na chombo kitatokea kwa mtakasaji;
5 Mwondoe asiye haki mbele ya mfalme, Na kiti chake cha enzi kitathibitika katika haki.
6 Usijitukuze mbele ya uso wa mfalme; Wala usisimame mahali pa watu wakuu;
7 Kwa maana ni heri kuambiwa, Njoo huku mbele; Kuliko kuwekwa nyuma machoni pa mkuu. Yale uliyoyaona kwa macho,
8 Usitoke nje kwa haraka ili kuyashindania; Usije ukakosa kujua la kutenda hatimaye, Mwenzako atakapokuwa amekuaibisha.
9 Ujitetee na mwenzako peke yake; Bali usiifunue siri ya mtu mwingine;
10 Yeye asikiaye asije akakutukana; Na aibu yako isiondoke.
11 Neno linenwalo wakati wa kufaa, Ni kama machungwa katika vyano vya fedha.
12 Kipuli cha dhahabu, na pambo la dhahabu safi; Ndivyo alivyo mwonyaji mwenye hekima kwa sikio lisikialo.
13 Kama baridi ya theluji wakati wa mavuno; Ndivyo alivyo mjumbe mwaminifu kwao wamtumao; Kwa maana huwaburudisha bwana zake nafsi zao.
14 Kama mawingu na upepo pasipo mvua; Ndivyo alivyo yeye ajisifiaye karama kwa uongo.
15 Kwa uvumilivu mwingi mkuu husadikishwa; Na ulimi laini huvunja mfupa.
16 Je! Umeona asali? Kula kadiri ya kukutosha; Usije ukashiba na kuitapika.
17 Mguu wako usiingie katika nyumba ya jirani yako ila kwa kiasi; Asije akakukinai na kukuchukia.
18 Mtu amshuhudiaye jirani yake uongo Ni nyundo, na upanga, na mshale mkali.
19 Kumtumaini asiye mwaminifu wakati wa taabu Ni kama jino lililovunjika, au mguu ulioteguka.
20 Amwimbiaye nyimbo mtu mwenye moyo mzito, Ni kama yeye avuaye nguo wakati wa baridi; Ni kama siki juu ya magadi.
21 Adui yako akiwa ana njaa, mpe chakula; Tena akiwa ana kiu, mpe maji ya kunywa;
22 Maana utatia makaa ya moto kichwani pake; Na Bwana atakupa thawabu.
23 Upepo wa kusi huleta mvua; Vile vile asingiziaye huleta uso wa ghadhabu.
24 Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi.
25 Kama vile maji ya baridi kwa mtu mwenye kiu, Ndivyo ilivyo habari njema itokayo katika nchi ya mbali.
26 Mwenye haki amwangukiapo mtu mbaya Ni kama chemchemi iliyochafuka, Na kisima kilichokanyagwa.
27 Haifai kula asali nyingi mno; Vile vile mtu kutafuta utukufu wake mwenyewe si utukufu.
28 Asiyetawala roho yake Ni mfano wa mji uliobomolewa, usio na kuta.