Mlango 15
1 Ikawa baada ya hayo, Absalomu akajiwekea tayari gari na farasi, na watu hamsini wa kupiga mbio mbele yake.
2 Tena Absalomu huondoka asubuhi na mapema, na kusimama kando ya njia ya lango; kisha ikawa, mtu ye yote aliyekuwa na neno, lililokuwa halina budi kufika kwa mfalme ili kuhukumiwa, Absalomu humwita mtu huyo kwake, na kumwuliza, Wewe u mtu wa mji gani? Naye akasema, Mtumwa wako ni mtu wa kabila fulani ya Israeli.
3 Naye Absalomu humwambia, Tazama, maneno yako ni mema yenye haki; lakini hapana mtu aliyeagizwa na mfalme kukusikiliza.
4 Tena Absalomu husema, Laiti mimi ningewekwa kuwa mwamuzi katika nchi hii, ili kila mtu mwenye neno au daawa aje kwangu, nimpatie haki yake!
5 Tena ikawa hapo alipokaribia mtu ye yote kumsujudia, hunyosha mkono wake, na kumshika, na kumbusu.
6 Hivyo ndivyo Absalomu alivyowatendea Israeli wote, waliomwendea mfalme ili wapate hukumu; na hivyo Absalomu akawadanganya watu wa Israeli.
7 Hata ikawa mwisho wa miaka minne, Absalomu akamwambia mfalme Tafadhali uniache niende nikaondoe nadhiri yangu, niliyomwekea Bwana huko Hebroni.
8 Maana mimi mtumishi wako naliweka nadhiri hapo nilipokuwa nikikaa Geshuri katika Shamu, nikasema, Kama Bwana akinirudisha Yerusalemu kweli, ndipo nitamtumikia Bwana.
9 Naye mfalme akamwambia, Enenda na amani. Basi akaondoka, akaenda Hebroni.
10 Lakini Absalomu akapeleka wapelelezi katika kabila zote za Israeli kusema, Mara mtakaposikia sauti ya tarumbeta, ndipo mtakaposema Absalomu anamilikl huko Hebroni.
11 Na watu mia mbili walioalikwa wakatoka Yerusalemu pamoja na Absalomu, wakaenda katika ujinga wao wasijue neno lo lote.
12 Absalomu naye akatuma kumwita Ahithofeli Mgiloni, mshauri wake Daudi, kutoka katika mji wake, yaani, Gilo, alipokuwa akitoa dhabihu. Fitina yao ikawa na nguvu; maana watu waliokuwa pamoja na Absalomu wakazidi kuwa wengi.
13 Mjumbe akamfikilia Daudi, akasema, Mioyo ya watu wa Israeli inashikamana na Absalomu.
14 Basi Daudi akawaambia watumishi wake wote waliokuwa pamoja naye Yerusalemu, Ondokeni, tukakimbie kwa kuwa tusipokimbia hapana mtu miongoni mwetu atakayeokoka mikononi mwa Absalomu; haya! Fanyeni haraka, tuondoke, asitupate kwa upesi, na kutuletea maovu, na kuupiga mji huu kwa makali ya upanga.
15 Hao watumishi wa mfalme wakamwambia mfalme, Angalia, sisi watumishi wako tu tayari kutenda lo lote atakalolichagua bwana wetu mfalme.
16 Basi mfalme akatoka na watu wa nyumbani mwake wote wakafuatana naye. Mfalme akaacha wanawake kumi, masuria, ili kuitunza nyumba.
17 Mfalme akatoka, na watu wote wakamfuata; wakakaa kidogo katika Beth-merhaki.
18 Watumishi wake wote wakapita karibu naye; na Wakerethi wote, na Wapelethi wote, na Wagiti wote, watu mia sita walioandamana naye kutoka Gathi, wakapita mbele ya mfalme.
19 Ndipo mfalme akamwambia Itai, Mgiti, Mbona wewe unakwenda pamoja nasi? Rudi, ukakae na mfalme; maana wewe u mgeni, tena u mtu uliyefukuzwa mahali pako mwenyewe.
20 Kwa kuwa umekuja jana tu kwa nini nikusumbue leo, na kukuzungusha huko na huko pamoja nasi nami hapa naenda niwezapo kwenda? Rudi wewe, ukawarudishe na ndugu zako; rehema na kweli ziwe pamoja nawe.
21 Naye Itai akamjibu mfalme akasema, Kama aishivyo Bwana, na bwana wangu mfalme aishivyo, hakika yake kila mahali atakapokuwapo mfalme, bwana wangu, ikiwa ni kwa kufa au ikiwa ni kwa kuishi, ndipo atakapokuwapo na mtumwa wako.
22 Basi Daudi akamwambia Itai, Haya, enenda ukavuke. Akavuka Itai, Mgiti na watu wake wote, na watoto wadogo wote waliokuwa pamoja naye.
23 Na nchi yote ikalia kwa sauti kuu, nao watu wote wakavuka, mfalme mwenyewe naye akavuka kile kijito Kidroni, na hao watu wote wakavuka, wakielekea njia ya nyika.
24 Na tazama, Sadoki naye akaja, na Walawi wote pamoja naye, huku wakilichukua sanduku la agano la Mungu; kisha wakalitua hilo sanduku la Mungu; Abiathari naye akapanda juu, hata watu wote walipokwisha kuutoka mji.
25 Naye mfalme akamwambia Sadoki, Rudisha sanduku la Mungu mjini; nikipata kibali machoni pa Bwana atanirudisha, na kunionyesha tena sanduku hili, na maskani yake;
26 lakini akisema kama hivi, Mimi si radhi nawe kabisa; basi, mimi hapa, na anitendee kama aonavyo kuwa vyema.
27 Kisha mfalme akamwambia Sadoki, kuhani, Angalia, rudini mjini kwa amani, na wana wenu wawili pamoja nanyi,Ahimaasi,mwana wako, na Yonathani,mwana wa Abiathari.
28 Angalia, mimi nitangoja penye vivuko vya jangwani, hata litakaponifikilia neno la kunipasha habari kutoka kwenu.
29 Basi Sadoki na Abiathari wakalichukua sanduku la Mungu, wakalirudisha Yerusalemu; wakakaa huko.
30 Daudi akapanda akishika njia ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akilia alipokuwa akipanda; naye alikuwa amejifunika kichwa chake, akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia walipopanda.
31 Mtu mmoja akamwambia Daudi ya kwamba, Ahithofeli yu katika hao waliopatana na Absalomu; Daudi akasema, Ee Bwana, nakusihi, uligeuze shauri la Ahithofeli liwe ubatili.
32 Ikawa, Daudi alipofika juu, hapo Mungu alipoabudiwa, tazama, Hushai, Mwarki, akaja kumlaki na joho lake limeraruliwa, tena ana udongo kichwani mwake.
33 Daudi akamwambia, Ukienda mbele pamoja nami, utakuwa mzigo kwangu;
34 lakini ukirudi mjini, na kumwambia Absalomu, Nitakuwa mtumishi wako, Ee mfalme; kama vile nilivyokuwa mtumishi wa baba yako tokea zamani, ndivyo nitakavyokuwa mtumishi wako sasa; ndipo utayavunja mashauri ya Ahithofeli kwa ajili yangu.
35 Je! Hawako Sadoki na Abiathari, makuhani, pamoja nawe huko? Basi itakuwa, kila neno utakalolisikia katika jumba la mfalme, utawaambia Sadoki na Abiathari, makuhani.
36 Angalia, wanao huko pamoja nao wana wao wawili, Ahimaasi, mwana wa Sadoki, na Yonathani, mwana wa Abiathari; nanyi kwa mikono yao mtanipelekea habari ya kila neno mtakalolisikia.
37 Basi Hushai, rafiki wa Daudi, akaingia ndani ya mji; naye Absalomu akafika akaingia Yerusalemu.