Mlango 14
1 Baada ya siku mbili ilikuwa sikukuu ya Pasaka, na mikate isiyochachwa; wakuu wa makuhani na waandishi wakatafuta njia ya kumkamata kwa hila na kumwua.
2 Kwa maana walisema, Isiwe kwa wakati wa sikukuu, isije ikatokea ghasia katika watu.
3 Naye alipokuwapo Bethania, nyumbani mwa Simoni mkoma, ameketi chakulani, alikuja mwanamke mwenye kibweta cha marhamu ya nardo safi ya thamani nyingi; akakivunja kibweta akaimimina kichwani pake.
4 Palikuwa na watu waliochukizwa katika nafsi zao wakisema, Kwani kupoteza marhamu namna hii?
5 Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa dinari mia tatu na kuzidi, wakapewa maskini. Wakamnung'unikia sana yule mwanamke.
6 Yesu akasema, Mwacheni; mbona mnamtaabisha? Amenitendea kazi njema;
7 maana sikuzote mnao maskini pamoja nanyi, na kila mpendapo mwaweza kuwatendea mema; lakini mimi hamnami sikuzote.
8 Ametenda alivyoweza; ametangulia kuupaka mwili wangu marhamu kwa ajili ya maziko.
9 Amin, nawaambia, Kila ihubiriwapo Injili katika ulimwengu wote, na hili alilotenda huyu litatajwa kwa kumbukumbu lake.
10 Yuda Iskariote, yule mmoja katika wale Thenashara, akaenda zake kwa wakuu wa makuhani, apate kumsaliti kwao.
11 Nao waliposikia walifurahi, wakaahidi kumpa fedha. Akatafuta njia ya kumsaliti wakati wa kufaa.
12 Hata siku ya kwanza ya mikate isiyochachwa, walipoichinja pasaka, wanafunzi wake wakamwambia, Ni wapi utakapo tuende tukuandalie uile pasaka?
13 Akatuma wawili katika wanafunzi wake, akawaambia, Nendeni zenu mjini; atakutana nanyi mwanamume amechukua mtungi wa maji; mfuateni;
14 na po pote atakapoingia, mwambieni mwenye nyumba, Mwalimu asema, Ki wapi chumba changu cha wageni, niile pasaka humo, pamoja na wanafunzi wangu?
15 Naye mwenyewe atawaonyesha orofa kubwa, imeandikwa tayari; humo tuandalieni.
16 Wanafunzi wakatoka, wakaenda mjini, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa pasaka.
17 Basi ilipokuwa jioni yuaja pamoja na wale Thenashara.
18 Nao walipokuwa wameketi chakulani, wakila, Yesu alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu, naye anakula pamoja nami, atanisaliti.
19 Wakaanza kuhuzunika, wakamwambia mmoja mmoja, Je! Ni mimi?
20 Akawaambia, Ni mmoja wa hao Thenashara, ambaye achovya pamoja nami katika kombe.
21 Kwa maana Mwana wa Adamu aenda zake kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu; ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa.
22 Nao walipokuwa wakila, alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa, akasema, Twaeni; huu ndio mwili wangu.
23 Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa; wakakinywea wote.
24 Akawaambia, Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi.
25 Amin, nawaambia ninyi, Sitakunywa tena kabisa uzao wa mzabibu, hata siku ile nitakapounywa mpya katika ufalme wa Mungu.
26 Nao walipokwisha kuimba walitoka kwenda mlima wa Mizeituni.
27 Yesu akawaambia, Mtakunguwazwa ninyi nyote kwa ajili yangu usiku huu; kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo watatawanyika.
28 Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.
29 Petro akamwambia, Hata wajapokunguwazwa wote, lakini siyo mimi.
30 Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, Leo, usiku huu, kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu.
31 Naye akazidi sana kusema, Ijaponipasa kufa nawe, hata hivyo sitakukana kamwe. Na wote wakasema vile vile.
32 Kisha wakaja mpaka bustani iitwayo Gethsemane; akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa muda niombapo.
33 Akamtwaa Petro na Yakobo na Yohana pamoja naye, akaanza kufadhaika sana na kuhangaika.
34 Akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa mkeshe.
35 Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akiomba ya kuwa, ikiwezekana, saa hiyo imwepuke.
36 Akasema, Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.
37 Akaja akawakuta wamelala usingizi, akamwambia Petro, Je! Simoni, umelala? Hukuweza kukesha saa moja?
38 Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi ila mwili ni dhaifu.
39 Akaenda zake tena, akaomba, akisema neno lilo hilo.
40 Akaja tena akawakuta wamelala, maana macho yao yamekuwa mazito, wala hawakujua la kumjibu.
41 Akaja mara ya tatu, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike; yatosha, saa imekuja; tazama, Mwana wa Adamu anatiwa mikononi mwao wenye dhambi.
42 Ondokeni, twendeni zetu; tazama, yule anayenisaliti amekaribia.
43 Basi alipokuwa katika kusema, mara Yuda alifika, mmoja wa wale Thenashara, na pamoja naye mkutano, wana panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee.
44 Na yule anayemsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni, mkamchukue salama.
45 Basi alipokuja, mara akamwendea, akasema, Rabi, akambusu.
46 Wakanyosha mikono yao wakamkamata.
47 Na mmoja wao waliokuwapo akafuta upanga, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio.
48 Yesu akajibu, akawaambia, Je! Ni kama juu ya mnyang'anyi mmetoka wenye panga na marungu, kunitwaa mimi?
49 Kila siku nalikuwa mbele yenu hekaluni nikifundisha, msinikamate; lakini haya yamekuwa ili maandiko yapate kutimia.
50 Ndipo wakamwacha, wakakimbia wote.
51 Na kijana mmoja alimfuata, amejitanda mwili wake nguo ya kitani; wakamkamata;
52 naye akaiacha ile nguo ya kitani, akakimbia yu uchi.
53 Nao wakamchukua Yesu kwa Kuhani Mkuu; wakamkusanyikia wote, wakuu wa makuhani na wazee na waandishi.
54 Naye Petro akamfuata kwa mbali, hata ndani katika behewa ya Kuhani Mkuu; akawa ameketi pamoja na watumishi, anakota moto mwangani.
55 Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda juu ya Yesu wapate kumwua; wasione.
56 Kwa maana wengi walimshuhudia uongo, walakini ushuhuda wao haukupatana.
57 Hata wengine wakasimama, wakamshuhudia uongo, wakisema,
58 Sisi tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono.
59 Wala hata hivi ushuhuda wao haukupatana.
60 Kisha Kuhani Mkuu akasimama katikati, akamwuliza Yesu, akisema, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini?
61 Lakini akanyamaza, wala hakujibu neno. Kuhani Mkuu akamwuliza tena, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wake Mtukufu?
62 Yesu akasema, Mimi ndiye, nanyi mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija na mawingu ya mbinguni.
63 Kuhani Mkuu akararua nguo zake, akisema, Tuna haja gani tena ya mashahidi?
64 Mmesikia kufuru yake; mwaonaje ninyi? Wote wakamhukumu kuwa imempasa kuuawa.
65 Wengine wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, na kumpiga makonde, na kumwambia, tabiri. Hata watumishi nao wakampiga makofi.
66 Na Petro alikuwa chini behewani; akaja mmoja wa vijakazi wa Kuhani Mkuu,
67 akamwona Petro akikota moto; akamkazia macho, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na yule Mnazareti, Yesu.
68 Akakana, akasema, Sijui wala sisikii unayoyasema wewe. Akatoka nje hata ukumbini; jogoo akawika.
69 Na yule kijakazi akamwona tena, akaanza tena kuwaambia waliosimama pale, Huyu ni mmoja wao.
70 Akakana tena. Kitambo kidogo tena wale waliosimama pale wakamwambia Petro, Hakika u mmoja wao, kwa sababu u Mgalilaya wewe.
71 Akaanza kulaani na kuapiza, Simjui mtu huyu mnayemnena.
72 Na mara jogoo akawika mara ya pili. Petro akalikumbuka lile neno aliloambiwa na Yesu, Kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu. Na alipolifikiri, akalia.