Mlango 13
1 Hata alipokuwa akitoka hekaluni, mmoja wa wanafunzi wake alimwambia, Mwalimu, tazama, yalivyo mawe na majengo haya!
2 Yesu akajibu, akamwambia, Wayaona majengo haya makubwa? Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomolewa.
3 Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, kuelekea hekalu Petro, na Yakobo, na Yohana, na Andrea walimwuliza kwa faragha,
4 Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya wakati, hayo yote yatakapokuwa karibu kutimia?
5 Yesu akaanza kuwaambia, Jihadharini, mtu asiwadanganye.
6 Wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye, nao watadanganya wengi.
7 Nanyi mtakaposikia habari za vita na uvumi wa vita, msitishwe; hayo hayana budi kutukia, lakini ule mwisho bado.
8 Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na matetemeko ya nchi mahali mahali; kutakuwako na njaa; hayo ndiyo mwanzo wa utungu.
9 Nanyi jihadharini nafsi zenu; maana watawapeleka ninyi mabarazani; na katika masinagogi mtapigwa; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao.
10 Na sharti Injili ihubiriwe kwanza katika mataifa yote.
11 Na watakapowachukua ninyi, na kuwasaliti, msitafakari kwanza mtakayosema, lakini lo lote mtakalopewa saa ile, lisemeni; kwa maana si ninyi msemao, bali ni Roho Mtakatifu.
12 Na ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, na baba atamsaliti mtoto, na watoto watashambulia wazazi wao, na kuwafisha.
13 Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kusaburi hata mwisho, ndiye atakayeokoka.
14 Lakini mlionapo chukizo la uharibifu likisimama pasipolipasa, (asomaye na afahamu), ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani;
15 na mtu aliye juu ya dari asishuke, wala asiingie kuchukua kitu nyumbani mwake;
16 naye aliye shambani asirudi nyuma kulichukua vazi lake.
17 Lakini ole wao wenye mimba, nao wanyonyeshao siku hizo!
18 Ila ombeni yasitokee hayo wakati wa baridi.
19 Kwa maana siku hizo zitakuwa na dhiki, jinsi isivyokuwa tangu mwanzo wa kuumba alipoumba Mungu hata sasa, wala haitakuwa kamwe.
20 Na kama Bwana asingalizikatiza siku hizo, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule aliowateua amezikatiza siku hizo.
21 Na wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule, msisadiki;
22 kwa maana wataondoka Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, watatoa ishara na maajabu, wapate kuwadanganya, kama yamkini, hata hao wateule.
23 Bali ninyi jihadharini; nimekwisha kuwaonya yote mbele.
24 Lakini siku zile, baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza, na mwezi hatautoa mwanga wake.
25 na nyota za mbinguni zitakuwa zikianguka, na nguvu zilizo mbinguni zitatikisika.
26 Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu.
27 Ndipo atakapowatuma malaika na kuwakusanya wateule wake toka pepo nne, toka upande wa mwisho wa nchi hata upande wa mwisho wa mbingu.
28 Kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake liishapo kuwa laini, na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno ni karibu;
29 nanyi kadhalika, myaonapo mambo hayo yanaanza, tambueni ya kuwa yu karibu milangoni.
30 Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatimie.
31 Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
32 Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba.
33 Angalieni, kesheni, [ombeni], kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo.
34 Mfano wake ni kama mtu mwenye kusafiri, ameiacha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri, na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe.
35 Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo bwana wa nyumba, kwamba ni jioni, au kwamba ni usiku wa manane, au awikapo jimbi, au asubuhi;
36 asije akawasili ghafula akawakuta mmelala.
37 Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, Kesheni.