Mlango 10
1 Ee Bwana, kwa nini wasimama mbali? Kwani kujificha nyakati za shida?
2 Kwa kiburi chake asiye haki mnyonge anafuatiwa kwa ukali; Na wanaswe kwa hila zizo hizo walizoziwaza.
3 Maana mdhalimu hujisifia tamaa ya nafsi yake, Na mwenye choyo humkana Bwana na kumdharau.
4 Mdhalimu kwa kiburi cha uso wake Asema, Hatapatiliza. Jumla ya mawazo yake ni, Hakuna Mungu;
5 Njia zake ni thabiti kila wakati. Hukumu zako ziko juu asizione, Adui zake wote awafyonya.
6 Asema moyoni mwake, Sitaondoshwa, Kizazi baada ya kizazi sitakuwamo taabuni.
7 Kinywa chake kimejaa laana, Na hila na dhuluma. Chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu,
8 Hukaa katika maoteo ya vijiji. Mahali pa siri humwua asiye na hatia, Macho yake humvizia mtu duni.
9 Huotea faraghani kama simba pangoni, Huotea amkamate mtu mnyonge. Naam, humkamata mtu mnyonge, Akimkokota wavuni mwake.
10 Hujikunyata na kuinama; Watu duni huanguka kwa nguvu zake.
11 Asema moyoni mwake, Mungu amesahau, Auficha uso wake, haoni kamwe.
12 Bwana, uondoke, Ee Mungu, uuinue mkono wako, Usiwasahau wanyonge.
13 Kwani mdhalimu kumdharau Mungu. Akisema moyoni mwake, Hutapatiliza?
14 Umeona, maana unaangalia madhara na jeuri, Uyatwae mkononi mwako. Mtu duni hukuachia nafsi yake, Maana umekuwa msaidizi wa yatima.
15 Uuvunje mkono wake mdhalimu, Na mbaya, uipatilize dhuluma yake, hata usiione.
16 Bwana ndiye Mfalme milele na milele; Mataifa wamepotea kutoka nchi yake.
17 Bwana, umeisikia tamaa ya wanyonge, Utaitengeneza mioyo yao, utalitega sikio lako.
18 Ili kumhukumu yatima naye aliyeonewa, Binadamu aliye udongo asizidi kudhulumu.