Mlango 40
1 Bwana akafuliza kumjibu Ayubu, na kusema,
2 Je! Mwenye hoja atashindana na Mwenyezi? Mwenye kujadiliana na Mungu, na ajibu yeye.
3 Ndipo Ayubu akamjibu Mungu, na kusema,
4 Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu.
5 Nimenena mara moja, nami sitajibu; Naam, nimenena mara mbili, lakini sitaendelea zaidi.
6 Ndipo Bwana akamjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema,
7 Jifunge viuno kama mwanamume, Mimi nitakuuliza neno, nawe niambie.
8 Je! Hata hukumu yangu utaibatilisha? Utanitia mimi hatiani, upate kuhesabiwa haki?
9 Au je! Wewe una mkono kama Mungu? Waweza kutoa ngurumo kwa sauti kama yeye?
10 Haya! Jivike sasa fahari na ukuu; Jipambe heshima na enzi.
11 Mwaga mafuriko ya hasira zako, Ukamtazame kila mtu mwenye kiburi, ukamdhili.
12 Mtazame kila mtu mwenye kiburi ukamshushe, Ukawakanyage waovu hapo wasimamapo.
13 Wafiche mavumbini pamoja, Wafunge nyuso zao mahali palipositirika.
14 Ndipo mimi nami nitazikiri habari zako, Ya kuwa mkono wako wa kuume waweza kukuokoa.
15 Mwangalie huyo kiboko, niliyemwumba pamoja nawe; Yeye hula nyasi kama vile ng'ombe,
16 Tazama basi, nguvu zake ni katika viuno vyake, Na uwezo wake u katika mishipa ya tumbo lake.
17 Yeye hutikisa mkia wake mfano wa mwerezi; Mishipa ya mapaja yake yanaungamana pamoja.
18 Mifupa yake ni kama mirija ya shaba; Mbavu zake ni kama vipande vya chuma.
19 Yeye ni mkuu wa njia za Mungu; Yeye aliyemfanya alimpa upanga wake.
20 Hakika milima humtolea chakula; Hapo wachezapo wanyama wote wa barani.
21 Hulala chini ya miti yenye vivuli, Mafichoni penye mianzi, na matopeni.
22 Hiyo miti yenye vivuli humfunika kwa vivuli vyao; Mierebi ya vijito humzunguka.
23 Tazama, mto ukifurika, yeye hatetemeki; Hujiona yu salama, ijapokuwa Yordani hufurika hata kinywani pake.
24 Je! Mtu ye yote atamnasa akiwa yu macho, Au, kumtoboa pua yake kwa mtego?