Mlango 21
1 Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,
2 Yasikizeni sana maneno yangu; Jambo hili na liwe faraja yenu.
3 Niacheni, nami pia nitanena; Tena nikiisha nena, zidini kudhihaki.
4 Mimi, je! Mashitaka yangu yamhusu mwanadamu? Nami kwa nini nisikose kusubiri?
5 Niangalieni, mkastaajabu, Mkaweke mkono kinywani.
6 Hata nikumbukapo nahuzunika, Na utisho wanishika mwilini mwangu.
7 Mbona waovu wanaishi, Na kuwa wazee, naam, na kuongezeka kuwa na nguvu?
8 Kizazi chao kinathibitika nao machoni pao, Na wazao wao mbele ya macho yao.
9 Nyumba zao zi salama pasina hofu, Wala fimbo ya Mungu haiwapigi.
10 Fahali wao huvyaza wala hapungukiwi na nguvu; Ng'ombe wao mke huzaa, asiharibu mimba.
11 Huwatoa kama kundi watoto wao. Na watoto wao hucheza.
12 Huimba kwa matari na kwa kinubi, Na kuifurahia sauti ya filimbi.
13 Siku zao hutumia katika kufanikiwa, Kisha hushuka kuzimuni ghafula.
14 Walakini walimwambia Mungu. Tuondokee; Kwani hatutaki kuzijua njia zako.
15 Huyo Mwenyezi ni nani, hata tumtumikie? Nasi tutafaidiwa nini tukimwomba?
16 Tazama, kufanikiwa kwao hakumo mkononi mwao; Mashauri ya waovu na yawe mbali nami.
17 Je! Ni mara ngapi taa yao waovu huzimishwa? Na msiba wao kuwajilia? Na Mungu kuwagawanyia uchungu kwa hasira yake?
18 Ili wawe kama mabua makavu mbele ya upepo, Kama makapi yaliyochukuliwa na dhoruba?
19 Mwasema, Mungu huwawekea watoto wa mtu huo uovu wake. Na amlipe mwenyewe, ili apate kuujua.
20 Macho yake mwenyewe na yaone uharibifu wake, Akanywe ghadhabu zake Mwenyezi.
21 Kwani ana furaha gani katika mbari yake baada yake, Hesabu ya miezi yake itakapokwisha katwa katikati?
22 Je! Mtu awaye yote atamfundisha Mungu maarifa? Naye ndiye awahukumuye walioko juu.
23 Mmoja hufa katika nguvu zake kamili, Mwenye kukaa salama na kustarehe;
24 Vyombo vyake vimejaa maziwa, Na mafuta ya mifupani mwake ni laini.
25 Mwingine hufa katika uchungu wa roho, Asionje mema kamwe.
26 Wao hulala mavumbini sawasawa, Mabuu huwafunika.
27 Tazama, nayajua mawazo yenu, Na mashauri mnayoazimia kwa uovu juu yangu.
28 Kwa kuwa mwasema, Nyumba ya huyo mkuu i wapi? Na hema waliyoikaa hao waovu i wapi?
29 Je! Hamkuwauliza wapitao njiani? Na maonyo yao hamyajui?
30 Kwamba mwovu huachiliwa katika siku ya msiba? Na kuongozwa nje katika siku ya ghadhabu?
31 Ni nani atakayetangaza njia yake usoni pake? Tena ni nani atakayemlipa kwa hayo aliyofanya?
32 Pamoja na hayo atachukuliwa kaburini, Nao watalinda zamu juu ya ziara lake.
33 Udongo wa bondeni utakuwa tamu kwake, Na watu wote watafuata nyuma yake, Kama vile walivyomtangulia watu wasiohesabika.
34 Basi imekuwaje ninyi kunituza moyo bure, Kwa kuwa katika jawabu zenu unasalia uongo tu.