Mlango 4
1 Hata alipokufa Ehudi, wana wa Israeli wakafanya yaliyo maovu tena mbele za macho ya Bwana.
2 Bwana akawauza na kuwatia katika mkono wa Yabini, mfalme wa Kanaani, aliyetawala huko Hazori; na Sisera, aliyekaa katika Haroshethi wa Mataifa, alikuwa amiri wa jeshi lake.
3 Wana wa Israeli wakamlilia Bwana; kwa kuwa Sisera alikuwa na magari ya chuma mia kenda; naye akawaonea wana wa Israeli kwa nguvu muda wa miaka ishirini.
4 Basi Debora, nabii mke, mkewe Lapidothi, ndiye aliyekuwa mwamuzi wa Israeli wakati ule.
5 Naye alikaa chini ya mtende wa Debora, kati ya Rama na Betheli, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu; wana wa Israeli wakakwea kwake, awaamue.
6 Huyo akatuma mtu akamwita Baraka wa Abinoamu toka Kedesh-Naftali, akamwambia, Je! Bwana, Mungu wa Israeli, hakutoa amri, akisema, Enenda, ukawavute kwako, huko katika mlima wa Tabori, watu elfu kumi wa wana wa Naftali, na wa wana wa Zabuloni?
7 Nami nitakuvutia Sisera, amiri wa jeshi lake Yabini, hata mto wa Kishoni, pamoja na magari yake, na wingi wa watu wake; nami nitamtia mkononi mwako.
8 Baraka akamwambia, Kama utakwenda pamoja nami ndipo nitakwenda; bali kama huendi pamoja nami, mimi siendi.
9 Basi akasema, Hakika nitakwenda pamoja nawe, lakini safari utakayoiendea haitakupatia heshima wewe; maana Bwana atamwuza Sisera katika mkono wa mwanamke. Debora akainuka, akaenda pamoja na Baraka mpaka Kedeshi.
10 Baraka akawakutanisha Naftali na Zabuloni waende Kedeshi wakakwea watu elfu kumi wakimfuata; Debora naye akaenda pamoja naye.
11 Basi Heberi, Mkeni, alikuwa amejitenga na Wakeni, yaani na wana wa Hobabu, shemeji yake Musa, akaipiga hema yake mbali penye mwaloni ulioko Saanaimu, karibu na Kedeshi.
12 Watu wakamwambia Sisera ya kwamba Baraka, mwana wa Abinoamu amekwea kwenda mlima wa Tabori.
13 Sisera akayakusanya magari yake yote, naam, magari ya chuma mia kenda, na watu wote waliokuwa pamoja naye, toka Haroshethi wa Mataifa mpaka mto wa Kishoni.
14 Debora akamwambia Baraka, Haya! Inuka; maana siku hii ndiyo siku ambayo Bwana amemtia Sisera katika mkono wako. Je! Bwana hakutoka atangulie mbele yako? Basi Baraka akashuka katika mlima wa Tabori, na watu elfu kumi wakamfuata.
15 Bwana akamfadhaisha Sisera na magari yake yote, na jeshi lake lote, kwa makali ya upanga, mbele ya Baraka; basi Sisera akashuka katika gari lake, akakimbia kwa miguu.
16 Lakini Baraka akayafuatia magari, na jeshi, hata Haroshethi wa Mataifa; na hilo jeshi lote la Sisera likaanguka kwa makali ya upanga; hakusalia hata mtu mmoja.
17 Lakini Sisera akakimbia kwa miguu, akaifikilia hema ya Yaeli mkewe Heberi, Mkeni; kwa maana palikuwa na amani kati ya Yabini, mfalme wa Hazori, na nyumba ya Heberi, Mkeni.
18 Yaeli akatoka kwenda kumlaki Sisera, akamwambia, Karibu Bwana wangu, karibu kwangu; usiogope. Akakaribia kwake hemani, naye akamfunika kwa bushuti.
19 Akamwambia, Tafadhali nipe maji kidogo ninywe; maana nina kiu. Akafungua chupa ya maziwa, akampa kunywa, akamfunika.
20 Naye akamwambia, Simama mlangoni pa hema; kisha itakuwa mtu awaye yote akija na kukuuliza, akisema, Je! Yupo mtu hapa, basi, mjibu, La, hapana.
21 Ndipo Yaeli, mkewe Heberi, akatwaa kigingi cha hema, akashika nyundo mkononi mwake, akamwendea polepole, akamtia kile kigingi katika kipaji chake, nacho kikapenya, hata kuingia mchangani; kwa maana usingizi mzito ulikuwa umemshika; basi akazimia, akafa.
22 Na tazama, Baraka alipokuwa akimfuatia Sisera; Yaeli akatoka ili kumlaki, akamwambia, Njoo, nami nitakuonyesha yule mtu unayemtafuta. Basi akamwendea, na tazama, Sisera amelala humo, amekufa, na hicho kigingi kilikuwa kipajini mwake.
23 Basi hivyo Mungu akamshinda Yabini, mfalme wa Kanaani mbele ya wana wa Israeli siku hiyo.
24 Mkono wa wana wa Israeli ukazidi kupata nguvu juu ya Yabini, mfalme wa Kanaani, hata walipokuwa wamemwangamiza Yabini, mfalme wa Kanaani.