Mlango 2
1 Basi wewe, mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo katika Kristo Yesu.
2 Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine.
3 Ushiriki taabu pamoja nami, kama askari mwema wa Kristo Yesu.
4 Hakuna apigaye vita ajitiaye katika shughuli za dunia, ili ampendeze yeye aliyemwandika awe askari.
5 Hata mtu akishindana katika machezo hapewi taji, asiposhindana kwa halali.
6 Yampasa mkulima mwenye taabu ya kazi kuwa wa kwanza wa kupata fungu la matunda.
7 Yafahamu sana hayo nisemayo, kwa maana Bwana atakupa akili katika mambo yote.
8 Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili yangu.
9 Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi.
10 Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele.
11 Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana, Kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia;
12 Kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi;
13 Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.
14 Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa Mungu, wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana faida, bali huwaharibu wasikiao.
15 Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.
16 Jiepushe na maneno yasiyo na maana, ambayo si ya dini; kwa kuwa wataendelea zaidi katika maovu,
17 na neno lao litaenea kama donda-ndugu. Miongoni mwa hao wamo Himenayo na Fileto,
18 walioikosa ile kweli, wakisema ya kwamba kiyama imekwisha kuwapo, hata kuipindua imani ya watu kadha wa kadha.
19 Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake. Na tena, Kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu.
20 Basi katika nyumba kubwa havimo vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali na vya mti, na vya udongo; vingine vina heshima, vingine havina.
21 Basi ikiwa mtu amejitakasa kwa kujitenga na hao, atakuwa chombo cha kupata heshima, kilichosafishwa, kimfaacho Bwana, kimetengenezwa kwa kila kazi iliyo njema.
22 Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi.
23 Walakini uyakatae maswali ya upumbavu yasiyo na elimu, ukijua ya kuwa huzaa magomvi.
24 Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu;
25 akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli;
26 wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake.