Mlango 4
1 Ninyi akina bwana, wapeni watumwa wenu yaliyo haki na ya adili, mkijua ya kuwa ninyi nanyi mna Bwana mbinguni.
2 Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani;
3 mkituombea na sisi pia, kwamba Mungu atufungulie mlango kwa lile neno lake, tuinene siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake nimefungwa,
4 ili niidhihirishe, kama inipasavyo kunena.
5 Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati.
6 Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu.
7 Tikiko, ndugu mpendwa, mtumishi mwaminifu, mjoli wangu katika Bwana, atawaarifu mambo yangu yote;
8 ambaye nimemtuma kwenu kwa sababu iyo hiyo, ili mjue mambo yetu, naye akawafariji mioyo yenu;
9 pamoja na Onesimo, ndugu mwaminifu, mpendwa, aliye mtu wa kwenu. Hao watawaarifu mambo yote ya hapa petu.
10 Aristarko, aliyefungwa pamoja nami, awasalimu; na Marko, mjomba wake Barnaba, ambaye mmepokea maagizo kwa habari yake; akifika kwenu mkaribisheni.
11 Na Yesu aitwaye Yusto; hao ni watu wa tohara. Tena hao peke yao ni watendaji wa kazi pamoja nami kwa ajili ya ufalme wa Mungu; nao walikuwa faraja kwangu.
12 Epafra, aliye mtu wa kwenu, mtumwa wa Yesu Kristo, awasalimu, akifanya bidii siku zote kwa ajili yenu katika maombi yake, ili kwamba msimame wakamilifu na kuthibitika sana katika mapenzi yote ya Mungu.
13 Maana namshuhudia kwamba ana juhudi nyingi kwa ajili yenu, na kwa ajili ya hao walioko Laodikia, na kwa ajili ya hao walioko Hierapoli.
14 Luka, yule tabibu mpendwa, na Dema, wanawasalimu.
15 Wasalimuni ndugu walioko Laodikia, na Nimfa, na kanisa lililo katika nyumba yake.
16 Waraka huu ukiisha kusomwa kwenu fanyeni kwamba usomwe katika kanisa la Walaodikia pia; na ule wa Laodikia usomwe na ninyi.
17 Mwambieni Arkipo, Iangalie sana huduma ile uliyopewa katika Bwana, ili uitimize.
18 Salamu yangu mimi Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe. Kumbukeni kufungwa kwangu. Neema na iwe pamoja nanyi.