Mlango 2
1 Kisha, baada ya miaka kumi na minne, nalipanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na Barnaba, nikamchukua na Tito pamoja nami.
2 Nami nalikwenda kwa kuwa nalifunuliwa, nikawaeleza injili ile niihubiriyo katika Mataifa, lakini kwa faragha kwa hao walio wenye sifa, isiwe labda napiga mbio bure, au nalipiga mbio bure.
3 Lakini Tito aliyekuwa pamoja nami, naye ni Myunani, hakulazimishwa kutahiriwa.
4 Bali kwa ajili ya ndugu za uongo walioingizwa kwa siri; ambao waliingia kwa siri ili kuupeleleza uhuru wetu tulio nao katika Kristo Yesu, ili watutie utumwani;
5 ambao hata saa moja hatukujitia chini yao, ili kwamba kweli ya Injili ikae pamoja nanyi.
6 Lakini wale wenye sifa ya kuwa wana cheo; (walivyokuwa vyo vyote ni mamoja kwangu; Mungu hapokei uso wa mwanadamu); nasema, hao wenye sifa hawakuniongezea kitu;
7 bali, kinyume cha hayo, walipoona ya kuwa nimekabidhiwa injili ya wasiotahiriwa, kama vile Petro ya waliotahiriwa;
8 (maana yeye aliyemwezesha Petro kuwa mtume wa waliotahiriwa ndiye aliyeniwezesha mimi kwenda kwa Mataifa);
9 tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohana, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara;
10 ila neno moja tu walitutakia, tuwakumbuke maskini; nami neno lilo hilo nalikuwa na bidii kulifanya.
11 Lakini Kefa alipokuja Antiokia, nalishindana naye uso kwa uso, kwa sababu alistahili hukumu.
12 Kwa maana kabla hawajaja watu kadha wa kadha waliotoka kwa Yakobo, alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa; lakini walipokuja wao, akarudi nyuma akajitenga, huku akiwaogopa waliotahiriwa.
13 Na hao Wayahudi wengine wakajigeuza pamoja naye, hata na Barnaba pia akachukuliwa na unafiki wao.
14 Walakini, nilipoona ya kuwa njia yao haiendi sawasawa na ile kweli ya Injili, nalimwambia Kefa mbele ya wote, Ikiwa wewe uliye Myahudi wafuata desturi za Mataifa, wala si za Wayahudi, kwa nini unawashurutisha Mataifa kufuata desturi za Wayahudi?
15 Sisi tulio Wayahudi kwa asili, wala si wakosaji wa Mataifa,
16 hali tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu; sisi tulimwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki.
17 Lakini ikiwa sisi wenyewe, kwa kutafuta kuhesabiwa haki katika Kristo, tulionekana kuwa wenye dhambi, je! Kristo amekuwa mtumishi wa dhambi? Hasha!
18 Maana nikiyajenga tena yale niliyoyabomoa, naonyesha ya kuwa mimi mwenyewe ni mkosaji.
19 Maana mimi kwa njia ya sheria naliifia sheria ili nimwishie Mungu.
20 Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.
21 Siibatili neema ya Mungu; maana, ikiwa haki hupatikana kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure.