Mlango 16
1 Tena, aliwaambia wanafunzi wake, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyekuwa na wakili wake; huyu alishitakiwa kwake kuwa anatapanya mali zake.
2 Akamwita, akamwambia, Ni habari gani hii ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya uwakili wako, kwa kuwa huwezi kuwa wakili tena.
3 Yule wakili akasema moyoni mwake, Nifanyeje? Maana, bwana wangu ananiondolea uwakili. Kulima, siwezi; kuomba, naona haya.
4 Najua nitakalotenda, ili nitakapotolewa katika uwakili, wanikaribishe nyumbani mwao.
5 Akawaita wadeni wa bwana wake, kila mmoja; akamwambia wa kwanza, Wawiwani na bwana wangu?
6 Akasema, Vipimo mia vya mafuta. Akamwambia, Twaa hati yako, keti upesi, andika hamsini.
7 Kisha akamwambia mwingine, Na wewe wawiwani? Akasema, Makanda mia ya ngano. Akamwambia, Twaa hati yako, andika themanini.
8 Yule bwana akamsifu wakili dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru.
9 Nami nawaambia, Jifanyieni rafiki kwa mali ya udhalimu, ili itakapokosekana wawakaribishe katika makao ya milele.
10 Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia.
11 Basi, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli?
12 Na kama hamkuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe?
13 Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana, ama atamchukia huyu na kumpenda huyu, ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.
14 Basi Mafarisayo, ambao wenyewe ni wapenda fedha, waliyasikia hayo yote, wakamdhihaki.
15 Akawaambia, Ninyi ndinyi mnaojidai haki mbele ya wanadamu, lakini Mungu awajua mioyo yenu; kwa kuwa lililotukuka kwa wanadamu huwa chukizo mbele za Mungu.
16 Torati na manabii vilikuwapo mpaka Yohana; tangu wakati huo habari njema ya ufalme wa Mungu hutangazwa, na kila mtu hujiingiza kwa nguvu.
17 Lakini ni vyepesi zaidi mbingu na nchi vitoweke, kuliko itanguke nukta moja ya torati.
18 Kila amwachaye mkewe na kumwoa mke mwingine azini; naye amwoaye yeye aliyeachwa na mumewe azini.
19 Akasema, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa.
20 Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi,
21 naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake.
22 Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa.
23 Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake.
24 Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu.
25 Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa.
26 Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu.
27 Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu,
28 kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso.
29 Ibrahimu akasema, Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao.
30 Akasema, La, baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu.
31 Akamwambia, Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu.