Ezra

Mlango: 1 2 3 4 5 6 7 8 9 10


Mlango 6

1 Ndipo mfalme Dario akatoa amri, na watu wakatafuta katika nyumba ya vyuo vya tarehe, hapo akiba zilipowekwa katika Babeli.
2 Na chuo kimoja kilipatikana huko Akmetha, katika nyumba ya mfalme iliyo katika wilaya ya Umedi, na ndani yake maneno haya yameandikwa ili yakumbukwe.
3 Katika mwaka wa kwanza wa mfalme Koreshi, mfalme Koreshi alitoa amri, Kwa habari ya nyumba ya Mungu huko Yerusalemu, nyumba hiyo na ijengwe, mahali watoapo dhabihu, na misingi yake ipigwe na kufanywa imara sana; kuinuka kwake kuwe mikono sitini, na upana wake mikono sitini;
4 ziwepo safu tatu za mawe makubwa, na safu moja ya miti mipya; gharama zake zitolewe katika nyumba ya mfalme.
5 Na vyombo vya dhahabu na fedha, vya nyumba ya Mungu, ambavyo mfalme Nebukadreza alivitoa katika nyumba ya Mungu, iliyoko Yerusalemu, akavileta mpaka Babeli, na virudishwe, vikaingizwe tena katika hekalu lililoko Yerusalemu, kila kimoja mahali pake, na wewe uvitie katika nyumba ya Mungu.
6 Basi sasa ninyi, Tatenai, liwali wa ng'ambo ya Mto, na Shethar-Bozenai, na hao wenzi wenu wa Kiajemi, mlio ng'ambo ya Mto, jitengeni na mahali pale;
7 iacheni kazi hii ya nyumba ya Mungu, msiizuie; waacheni liwali wa Wayahudi, na wazee wa Wayahudi, waijenge nyumba hii ya Mungu mahali pake.
8 Tena, natoa amri kuwaagiza ninyi mtakayowatendea wazee hao wa Wayahudi, kwa kazi hii ya kuijenga nyumba ya Mungu; katika mali ya mfalme, yaani, katika kodi za nchi iliyo ng'ambo ya Mto, watu hao wapewe gharama zote kwa bidii, ili wasizuiliwe.
9 Na kila kitu wanachokihitaji, katika ng'ombe wachanga, na kondoo waume, na wana-kondoo, kwa sadaka za kuteketezwa watakazomtolea Mungu wa mbinguni, na ngano, na chumvi, na divai, na mafuta, kama makuhani walioko Yerusalemu watakavyosema, na wapewe vitu hivyo vyote siku kwa siku, msikose kuwapa;
10 wapate kumtolea Mungu wa mbinguni sadaka zenye harufu nzuri, na kumwombea mfalme, na wanawe, wapate uzima.
11 Pia nimetoa amri kwamba, mtu awaye yote atakayelibadili neno hili, boriti na itolewe katika nyumba yake, akainuliwe na kutungikwa juu yake; tena nyumba yake ikafanywe jaa kwa ajili ya neno hili.
12 Na Mungu huyu, aliyelifanya jina lake likae pale, na aangamize wafalme wote, na watu wote, watakaonyosha mikono yao kulibadili neno hili, na kuiharibu nyumba hii ya Mungu, iliyoko Yerusalemu. Mimi, Dario, nimetoa amri; na ifanyike kwa bidii nyingi.
13 Ndipo Tatenai, liwali wa ng'ambo ya Mto, na Shethar-Bozenai, na wenzi wao, wakafanya hayo kwa bidii, kwa sababu mfalme Dario alikuwa ametuma watu kwao.
14 Nao wazee wa Wayahudi wakajenga, wakafanikiwa, kwa msaada wa kuhubiri kwao Hagai nabii, na Zekaria mwana wa Ido. Wakajenga, wakaimaliza kazi yao, kwa maagizo ya Mungu wa Israeli, na kwa amri ya Koreshi, na Dario, na Artashasta mfalme wa Uajemi.
15 Nyumba hiyo ikamalizika siku ya tatu ya mwezi Adari, katika mwaka wa sita wa kutawala kwake mfalme Dario.
16 Na wana wa Israeli, na makuhani na Walawi, na watu wengine katika hao waliohamishwa, wakaiweka wakfu nyumba ya Mungu kwa furaha.
17 Na katika kuiweka wakfu nyumba ya Mungu, wakatoa sadaka, ng'ombe mia, na kondoo waume mia mbili, na wana-kondoo mia nne; tena wakatoa mbuzi waume kumi na wawili, kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili ya Israeli wote, kwa hesabu ya kabila za Israeli.
18 Wakawaweka makuhani katika kura zao, wakawaweka na Walawi katika zamu zao, kwa ajili ya huduma ya Mungu, iliyokuwako Yerusalemu; vile vile kama vilivyoandikwa katika chuo cha Musa.
19 Kisha, wana wa uhamisho wakaifanya Pasaka, mwezi wa kwanza siku ya kumi na nne ya mwezi.
20 Kwa maana makuhani na Walawi walikuwa wamejitakasa wote pamoja; wote walikuwa hali ya tohara; wakachinja Pasaka kwa ajili ya wana wote wa uhamisho, na kwa ajili ya ndugu zao makuhani, na kwa ajili ya nafsi zao.
21 Wana wa Israeli wakaila, wale waliorudi kuitoka nchi ya uhamisho wao, na watu wote ambao pamoja nao wamejitenga na uchafu wa taifa za nchi, ili kumtaka Bwana, Mungu wa Israeli,
22 wakaifanya sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu kwa furaha, kwa muda wa siku saba; kwa kuwa Bwana amewafurahisha, na kumgeuza moyo mfalme wa Ashuru, awaelekee, ili awatie nguvu mikono yao katika kazi hiyo ya nyumba ya Mungu, Mungu wa Israeli.