Mlango 6
1 Kisha, wana wa manabii wakamwambia Elisha, Angalia basi, mahali tukaapo mbele yako ni padogo kwetu.
2 Basi twende mpaka Yordani, twakuomba, tutwae huko kila mtu mti mmoja, ili tujifanyie huko mahali pa kukaa. Akajibu, Haya! Nendeni.
3 Mmoja wao akasema, Uwe radhi, basi nakusihi, uende pamoja na watumishi wako. Akajibu, Nitakwenda.
4 Basi, akaenda pamoja nao. Nao walipofika Yordani, wakakata miti.
5 Lakini mmojawapo alipokuwa katika kukata boriti, chuma cha shoka kikaanguka majini; akalia, akasema, Ole wangu! Bwana wangu, kwani kiliazimiwa kile.
6 Mtu wa Mungu akasema, Kilianguka wapi? Akamwonyesha mahali. Akakata kijiti, akakitupa pale pale, chuma kikaelea.
7 Akasema, Kiokote. Basi akanyosha mkono, akakitwaa.
8 Basi, mfalme wa Shamu alikuwa akifanya vita na Israeli. Akafanya mashauri na watumishi wake, akasema, Kituo changu kitakuwapo mahali fulani.
9 Yule mtu wa Mungu akapeleka habari kwa mfalme wa Israeli, kusema, Jihadhari, usipite mahali fulani; kwa sababu ndiko wanakoshukia Washami.
10 Mfalme wa Israeli akapeleka watu mpaka mahali pale alipoambiwa na yule mtu wa Mungu, na kuhadharishwa; akajiokoa nafsi yake, si mara moja, wala si mara mbili.
11 Basi mfalme wa Shamu moyo wake ukamfadhaika sana kwa ajili ya jambo hili; akawaita watumishi wake, akawaambia, Je! Hamtanionyesha, ni mtu yupi miongoni mwenu aliye upande wa mfalme wa Israeli?
12 Mmojawapo wa watumishi wake akasema, La, bwana wangu, mfalme; lakini Elisha, yule nabii aliye katika Israeli, humwambia mfalme wa Israeli maneno uyanenayo katika chumba chako cha kulala.
13 Akasema, Enendeni, mkamwangalie aliko, nipate kupeleka watu kwenda kumchukua. Akaambiwa ya kwamba, Tazama, yuko Dothani.
14 Kwa hiyo akapeleka huko farasi, na magari, na jeshi kubwa; wakafika usiku, wakauzingira mji ule pande zote.
15 Hata asubuhi na mapema mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje?
16 Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.
17 Elisha akaomba, akasema, Ee Bwana, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. Bwana akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote.
18 Na walipomtelemkia Elisha akamwomba Bwana, akasema, Uwapige, nakusihi, watu hawa kwa upofu. Akawapiga kwa upofu sawasawa na neno la Elisha.
19 Elisha akawaambia, Njia hii siyo, na mji huu sio, nifuateni mimi, nami nitawapeleka kwa mtu yule mnayemtafuta. Akawapeleka Samaria.
20 Hata walipokwisha kuingia Samaria, Elisha akasema, Bwana wafumbue macho watu hawa, wapate kuona. Bwana akawafumbua macho wakaona; kumbe! Walikuwa katikati ya Samaria.
21 Naye mfalme wa Israeli alipowaona, akamwambia Elisha, Ee baba yangu, niwapige? Niwapige?
22 Akamjibu, Usiwapige; je! Ungetaka kuwapiga watu ambao umewatwaa mateka kwa upanga wako na uta wako? Weka chakula na maji mbele yao, wapate kula na kunywa, na kwenda kwa bwana wao.
23 Basi akawaandalia chakula tele; nao walipokwisha kula na kunywa, akawaacha, wakaenda zao kwa bwana wao. Na vikosi vya Shamu havikuja tena katika nchi ya Israeli.
24 Ikawa baada ya hayo, Ben-hadadi mfalme wa Shamu akakusanya majeshi yake yote, akakwea akauhusuru Samaria.
25 Njaa ikawa kuu huko Samaria; na tazama, wakauhusuru, hata kichwa cha punda kikapata kuuzwa kwa vipande themanini vya fedha, na kibaba cha mavi ya njiwa kwa vipande vitano vya fedha.
26 Ikawa mfalme wa Israeli alipokuwa akipita ukutani, mwanamke mmoja akamwita akisema, Unisaidie, bwana wangu, mfalme.
27 Akasema, Bwana asipokusaidia, nikusaidieje mimi? Ya sakafuni, au ya shinikizoni?
28 Mfalme akamwambia, Una nini? Akajibu, Mwanamke huyu aliniambia, Mtoe mtoto wako, tumle leo, na mtoto wangu tutamla kesho.
29 Basi, tukamtokosa mtoto wangu, tukamla; nikamwambia siku ya pili, Mtoe mtoto wako, tumle; naye amemficha mtoto wake.
30 Ikawa, mfalme alipoyasikia maneno ya huyo mwanamke, aliyararua mavazi yake; (naye alikuwa akipita juu ya ukuta;) na watu wakaona, na tazama, alikuwa amevaa magunia ndani mwilini mwake.
31 Ndipo akasema, Mungu anifanyie hivyo, na kuzidi, kikimbakia kichwa Elisha mwana wa Shafati juu yake leo.
32 Lakini Elisha alikuwa akikaa nyumbani mwake, na wazee wakikaa pamoja naye; na mfalme akamtuma mtu wa mbele yake; lakini hata kabla ya kufika kwake yule aliyetumwa, akawaambia wazee, Je! Mwaona jinsi huyu mwana wa mwuaji alivyotuma aniondolee kichwa changu? Angalieni, huyo aliyetumwa akifika, fungeni mlango, mkamzuie mlangoni; je! Sauti ya miguu ya bwana wake haiko nyuma yake?
33 Hata alipokuwa katika kusema nao, tazama, yule aliyetumwa akamshukia; naye akasema, Angalia, mabaya haya yatoka kwa Bwana; kwani mimi kumngojea Bwana tena?