Mlango 2
1 Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema,
2 Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume;
3 uyashike mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako;
4 ili Bwana afanye imara neno lake alilonena kwa habari yangu, akisema, Ikiwa watoto wako wataiangalia njia yao, wakienda mbele zangu kwa kweli, kwa moyo wao wote, na kwa roho yao yote, (akasema), hutakosa mtu katika kiti cha enzi cha Israeli.
5 Na zaidi ya hayo, umejua alivyonitenda Yoabu, mwana wa Seruya, yaani, alivyowatenda majemadari wawili wa majeshi ya Israeli, Abneri, mwana wa Neri, na Amasa, mwana wa Yetheri, ambao aliwaua, na kuimwaga damu ya vita wakati wa amani, akautia damu ya vita mshipi uliokuwa viunoni mwake, na viatu vilivyokuwa miguuni mwake.
6 Kwa hiyo ufanye kama ilivyo hekima yako, wala usimwachie mvi zake kushukia Ahera kwa amani.
7 Lakini uwafanyie mema wana wa Barzilai Mgileadi, wawe miongoni mwao walao mezani pako; kwa jinsi walivyonijilia nilipokuwa nimekimbia mbele ya Absalomu, ndugu yako.
8 Hata, angalia, yuko pamoja nawe Shimei, mwana wa Gera, Mbenyamini, wa Bahurimu, ndiye aliyenilaani kwa laana kuu siku ile nilipokwenda Mahanaimu; lakini akashuka kunilaki kule Yordani, nami nikamwapia kwa Bwana, nikamwambia, Mimi sitakuua kwa upanga.
9 Basi kwa hiyo usimwachilie, kwa kuwa wewe u mtu wa akili; nawe utajua ikupasayo umtendee, na mvi zake utazishusha Ahera pamoja na damu.
10 Basi Daudi akalala na babaze, akazikwa mjini mwa Daudi.
11 Na siku alizotawala Daudi juu ya Israeli zilikuwa miaka arobaini; huko Hebroni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelathini na mitatu.
12 Basi Sulemani akaketi katika kiti cha enzi cha Daudi baba yake; na ufalme wake ukawa imara sana.
13 Ndipo Adonia mwana wa Hagithi akaja kwa Bath-sheba mamaye Sulemani. Naye akasema, Je! Umekuja kwa amani?
14 Naye akajibu, Kwa amani. Tena akasema, Nina shauri ninalotaka kukuambia. Naye akamwambia, Sema.
15 Basi akasema, Wajua ya kwamba ufalme ulikuwa wangu, na Israeli wote wakaniwekea nyuso zao ili nimiliki mimi; walakini sasa ufalme umegeuka kuwa wake ndugu yangu; kwa maana ulikuwa wake kutoka kwa Bwana.
16 Basi sasa nina haja moja ninayokuomba, usinikataze hiyo. Naye akamwambia, Sema.
17 Akasema, Nena, nakusihi, na Sulemani, mfalme, (kwa kuwa hawezi kukukataza neno), kwamba anioze Abishagi, Mshunami.
18 Naye Bath-sheba akasema, Vema; nitasema na mfalme kwa ajili yako.
19 Basi Bath-sheba akaingia kwa mfalme Sulemani, aseme naye kwa ajili ya Adonia. Naye mfalme akainuka kwenda kumlaki, akamwinamia, akaketi katika kiti chake cha enzi; kisha akaagiza awekewe kiti cha enzi mamaye mfalme; naye akaketi mkono wake wa kuume.
20 Ndipo akasema, Haja moja ndogo nakuomba; usinikataze. Mfalme akamwambia, Omba, mama; kwa kuwa siwezi kukukataza neno.
21 Naye akasema, Nataka Adonia, ndugu yako, aozwe Abishagi, Mshunami.
22 Akajibu mfalme Sulemani akamwambia mamaye, Na mbona wamtakia Adonia Abishagi, Mshunami? Umtakie na ufalme pia; kwa kuwa yeye ni ndugu yangu mkubwa; naam, umtakie yeye, na Abiathari kuhani, na Yoabu mwana wa Seruya.
23 Ndipo mfalme Sulemani akaapa kwa Bwana, akasema, Mungu anifanyie hivyo, na kuzidi, isipokuwa Adonia amenena neno hili juu ya uhai wake mwenyewe.
24 Basi kwa hiyo, Bwana aishivyo, aliyenithibitisha na kunikalisha katika kiti cha enzi cha Daudi baba yangu, akanifanyia nyumba, kama alivyoahidi, hakika atauawa leo hivi Adonia.
25 Mfalme Sulemani akatuma kwa mkono wa Benaya mwana wa Yehoyada: naye akampiga, hata akafa.
26 Tena, mfalme akamwambia Abiathari kuhani, Enenda Anathothi mashambani kwako; kwa kuwa wastahili kufa; ila leo sikuui, kwa sababu wewe ulichukua sanduku la Bwana mbele ya Daudi baba yangu, na kwa sababu wewe uliteswa kwa mateso yote ya baba yangu.
27 Hivyo Sulemani akamtoa Abiathari asiwe kuhani wa Bwana; ili alitimize neno la Bwana, alilonena juu ya nyumba ya Eli katika Shilo.
28 Tena, habari zikamfikia Yoabu; kwa maana Yoabu alikuwa amemfuata Adonia, ingawa hakumfuata Absalomu. Yoabu akakimbilia Hemani kwa Bwana, akazishika pembe za madhabahu.
29 Akaambiwa mfalme Sulemani ya kwamba, Yoabu amekimbilia Hemani kwa Bwana, naye, tazama, yuko madhabahuni. Ndipo Sulemani akamtuma Benaya, mwana wa Yehoyada, akisema, Enenda, umpige.
30 Basi Benaya akaja Hemani kwa Bwana, akamwambia, Mfalme asema hivi, Njoo utoke. Naye akajibu, La, sivyo; ila nitakufa papa hapa. Naye Benaya akamletea mfalme habari, akisema, Hivi ndivyo alivyonena Yoabu, na ndivyo alivyonijibu.
31 Mfalme akamwambia, Fanya alivyonena, umpige, ukamzike; ili uniondolee mimi na nyumba ya babangu damu aliyoimwaga Yoabu bure.
32 Naye Bwana atamrudishia damu yake kichwani pake mwenyewe, kwa kuwa aliwapiga watu wawili wenye haki, na wema kuliko yeye, akawaua kwa upanga, wala babangu Daudi hakujua habari hiyo; yaani Abneri, mwana wa Neri, jemadari wa jeshi la Israeli, na Amasa, mwana wa Yetheri, jemadari wa jeshi la Yuda.
33 Hivyo damu yao itarudi kichwani pa Yoabu, na kichwani pa wazao wake hata milele; ila kwa Daudi, na kwa wazao wake, na kwa nyumba yake, na kwa kiti chake cha enzi, kutakuwa na amani hata milele kutoka kwa Bwana.
34 Ndipo Benaya, mwana wa Yehoyada, akapanda, akampiga, akamwua; naye akazikwa katika nyumba yake mwenyewe iliyoko nyikani.
35 Kisha mfalme akamweka Benaya, mwana wa Yehoyada, mahali pake juu ya jeshi; na Sadoki, kuhani, mfalme akamweka mahali pa Abiathari.
36 Tena, mfalme akatuma watu akamwita Shimei, akamwambia, Ujijengee nyumba humu Yerusalemu, ukae ndani yake, wala usitoke humo kwenda mahali po pote.
37 Kwa kuwa siku ile ya kutoka kwako, na kuvuka kijito Kidroni, ujue hakika ya kwamba kufa utakufa; damu yako itakuwa juu ya kichwa chako mwenyewe.
38 Naye Shimei akamwambia mfalme, Neno hili ni jema; kama alivyosema bwana wangu mfalme, ndivyo atakavyofanya mtumwa wako. Basi Shimei akakaa Yerusalemu siku nyingi.
39 Ikawa miaka mitatu ilipokwisha, watumwa wawili wa Shimei wakatoroka kwenda kwa Akishi, mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi. Wakamwambia Shimei, wakasema, Angalia, watumwa wako wako huko Gathi.
40 Shimei akaondoka, akatandika punda wake, akaenda Gathi kwa Akishi, ili kuwatafuta watumwa wake. Akaenda Shimei, akawaleta watumwa wake toka Gathi.
41 Naye Sulemani akaambiwa, ya kwamba Shimei alikuwa ametoka Yerusalemu kwenda Gathi, na kurudi tena.
42 Basi, mfalme akatuma watu, akamwita Shimei, akamwambia, Je! Sikukuapisha kwa Bwana, na kukushuhudia, kusema, Siku ile ya kutoka kwako ukienda mahali po pote, ujue hakika ya kwamba kufa utakufa? Nawe ukaniambia, Neno hili nililolisikia ni jema?
43 Mbona basi hukukishika kiapo cha Bwana, na amri niliyokuagiza?
44 Tena, mfalme akamwambia Shimei, Umejua uovu wote uliouona moyoni mwako, uliomtenda Daudi baba yangu; basi kwa hiyo Bwana atakurudishia uovu wako kichwani pako mwenyewe.
45 Ila mfalme Sulemani atakuwa amebarikiwa, na kiti cha enzi cha Daudi kitathibitika mbele za Bwana hata milele.
46 Basi mfalme akamwamuru Benaya, mwana wa Yehoyada; naye akatoka, akampiga, hata akafa. Nao ufalme ukawa imara mkononi mwa Sulemani.