Mlango 17
1 Kisha hii ndiyo kura iliyoiangukia kabila ya Manase; maana, yeye alikuwa ni mzaliwa wa kwanza, wa Yusufu. Katika habari za Makiri, mzaliwa wa kwanza wa Manase, babaye Gileadi, kwa sababu alikuwa mtu wa vita, basi alikuwa na Gileadi na Bashani.
2 Na kura ilikuwa ni ya hao wana wa Manase waliosalia kwa kuandama jamaa zao; kwa wana wa Abiezeri, na kwa wana wa Heleki, na kwa wana wa Asrieli, na kwa wana wa Shekemu, na kwa wana wa Heferi, na kwa wana wa Shemida; hao ndio wana waume wa Manase, mwana wa Yusufu, kwa kuandama jamaa zao.
3 Lakini Selofehadi, mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, hakuwa na wana waume ila binti; na majina ya hao binti zake walikuwa wakiitwa Mala, na Noa, na Hogla, na Milka, na Tirsa.
4 Nao wakakaribia mbele ya Eleazari, kuhani, na mbele ya Yoshua, mwana wa Nuni, na mbele ya mashehe, wakasema, Bwana alimwamuru Musa kutupa sisi urithi kati ya ndugu zetu; basi kwa kuiandama hiyo amri ya Bwana akawapa urithi kati ya ndugu za baba yao.
5 Kisha kura zilizomwangukia Manase zilikuwa ni sehemu kumi, mbali na nchi ya Gileadi na Bashani, iliyo ng'ambo ya Yordani;
6 kwa sababu hao binti za Manase walikuwa na urithi katika wanawe waume; na nchi ya Gileadi ilikuwa ni mali ya hao wana waume wa Manase waliosalia.
7 Mpaka wa Manase ulikuwa kutoka Asheri hata Mikmeta, ulioelekea Shekemu; tena mpaka ukaendelea upande wa kuume, hata kuwafikilia wenyeji wa Entapua.
8 Hiyo nchi ya Tapua ilikuwa ni mali ya Manase; lakini ule mji wa Tapua uliokuwa katika mpaka wa Manase ulikuwa ni mali ya wana wa Efraimu.
9 Tena mpaka ulitelemkia mpaka kijito cha Kana, upande wa kusini wa hicho kijito; miji hiyo ilikuwa ya Efraimu kati ya miji ya Manase; na mpaka wa Manase ulikuwa upande wa kaskazini wa hicho kijito, na matokeo yake yalikuwa baharini;
10 upande wa kusini ilikuwa ni mali ya Efraimu, na upande wa kaskazini ilikuwa ni mali ya Manase, na bahari ilikuwa mpaka wake; nao wakafikilia hata Asheri upande wa kaskazini, na kufikilia hata Isakari upande wa mashariki.
11 Tena Manase alikuwa na miji katika Isakari na katika Asheri, nayo ni hii, Bethsheani na vijiji vyake, na Ibleamu na miji yake, na wenyeji wa Dori na miji yake, na wenyeji wa Endori na miji yake, na wenyeji wa Taanaki na miji yake, na wenyeji wa Megido na miji yake, hata mahali patatu palipoinuka.
12 Lakini wana wa Manase hawakuweza kuwafukuza wenyeji wa miji hiyo; bali hao Wakanaani walijikaza ili wakae katika nchi hiyo.
13 Kisha ikawa, hapo hao wana wa Israeli walipokuwa wamepata nguvu zaidi, ndipo wakawatenza nguvu hao Wakanaani wafanye kazi ya shokoa, wala hawakuwafukuza kabisa.
14 Kisha wana wa Yusufu wakanena na Yoshua, wakasema, Kwa nini umenipa mimi kura moja tu na fungu moja kuwa ni urithi wangu, kwa kuwa mimi ni taifa kubwa la watu, kwa sababu Bwana amenibarikia hata hivi sasa?
15 Yoshua akawaambia, Kwamba wewe u taifa kubwa la watu, haya, kwea uende mwituni, ujikatie mahali hapo kwa ajili ya nafsi yako katika nchi ya Waperizi, na ya hao Warefai; ikiwa hiyo nchi ya vilima ya Efraimu ni nyembamba, haikutoshi.
16 Wana wa Yusufu wakasema, Hiyo nchi ya vilima haitutoshi sisi; lakini Wakanaani wote wakaao katika nchi ya bondeni wana magari ya chuma, hao walio katika Bethsheani na miji yake, na hao walio katika bonde la Yezreeli pia.
17 Kisha Yoshua alinena na nyumba ya Yusufu, maana, ni Efraimu na Manase, akawaambia, Wewe u taifa kubwa la watu, nawe una uwezo mwingi; hutapata kura moja tu;
18 lakini hiyo nchi ya vilima itakuwa ni yako; maana, ijapokuwa ni mwitu, wewe utaukata, na matokeo yake yatakuwa ni yako; kwa kuwa wewe utawafukuza hao Wakanaani, wajapokuwa wana magari ya chuma, wajapokuwa ni wenye uwezo.