Mlango 15
1 Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,
2 Haya, semeni na wana wa Israeli, mkawaambie, Mtu ye yote atakapokuwa na kisonono kimtokacho mwilini mwake, atakuwa najisi kwa ajili ya kisonono chake.
3 Na unajisi wake katika kisonono chake ni huu; kama mwili wake unachuruzika kisonono chake, au kama kisonono chake kimezuiwa mwilini mwake, ni unajisi wake.
4 Kitanda cho chote akilaliacho mwenye kisonono kitakuwa najisi; na kitu cho chote ambacho akiketia kitakuwa najisi.
5 Mtu ye yote atakayekigusa kitanda chake huyo, atazifua nguo zake, na kuoga mwili wake majini, naye atakuwa najisi hata jioni.
6 Na mtu atakayeketi katika kitu cho chote alichokiketia mwenye kisonono, atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.
7 Na mtu atakayegusa mwili wake mwenye kisonono atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.
8 Tena kama mwenye kisonono akimtemea mate mtu aliye safi; ndipo atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa yu najisi hata jioni.
9 Na tandiko lo lote atakalolipanda mwenye kisonono litakuwa najisi.
10 Mtu awaye yote atakayegusa kitu cho chote kilichokuwa chini yake huyo atakuwa najisi hata jioni; na mtu atakayevichukua vitu vile atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.
11 Na mtu ye yote atakayeguswa na mwenye kisonono, asipokuwa amenawa mikono yake majini, atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.
12 Na chombo cha udongo ambacho amekigusa mwenye kisonono, kitavunjwa-vunjwa; na kila chombo cha mti kitaoshwa majini.
13 Na huyo aliye na kisonono atakapotakaswa na kisonono chake, atajihesabia siku saba kwa kutakaswa kwake, naye atazifua nguo zake; naye ataoga mwili wake katika maji ya mtoni, naye atakuwa safi.
14 Na siku ya nane atajipatia hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, naye atakwenda mbele za Bwana mlangoni pa hema ya kukutania, naye atampa kuhani hao ndege;
15 na kuhani atawasongeza, mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa; naye kuhani atafanya upatanisho mbele za Bwana kwa ajili ya kisonono chake.
16 Na mtu ye yote akitokwa na shahawa yake, ndipo ataoga mwili wake wote majini, naye atakuwa najisi hata jioni.
17 Na kila nguo, na kila ngozi, ambayo ina shahawa, itafuliwa kwa maji, nayo itakuwa najisi hata jioni.
18 Huyo mwanamke naye ambaye mtu mume amelala naye kwa shahawa, wote wawili wataoga majini, nao watakuwa najisi hata jioni.
19 Mwanamke ye yote, kama anatokwa na kitu, na kitu chake alichokuwa nacho mwilini mwake ni damu, ataketi katika kutengwa kwake muda wa siku saba; na mtu ye yote atakayemgusa atakuwa najisi hata jioni.
20 Na kitu cho chote akilaliacho katika kutengwa kwake kitakuwa najisi; na kila kitu ambacho akiketia kitakuwa najisi.
21 Mtu ye yote atakayekigusa kitanda chake huyo mwanamke atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.
22 Mtu ye yote atakayekigusa cho chote ambacho huyo mwanamke amekiketia atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.
23 Kwamba ni katika kitanda, au cho chote alichokikalia huyo mwanamke, atakapokigusa kitu hicho, atakuwa najisi hata jioni.
24 Na mtu ye yote atakayelala na mwanamke na unajisi ukawa juu yake, atakuwa najisi muda wa siku saba; na kila kitanda alichokilalia kitakuwa najisi.
25 Na mwanamke kama akitokwa na damu yake siku nyingi, nayo si katika majira ya kutengwa kwake, au kama anatoka damu kuzidi majira ya kutengwa kwake; siku hizo zote za kutoka damu ya unajisi wake, atakuwa kama alivyokuwa katika siku za kutengwa kwake; yeye yu najisi.
26 Kila kitanda akilaliacho katika siku zote za kutoka damu kitakuwa kama kitanda cha kutengwa kwake; na kila kitu atakachokilalia kitakuwa najisi, kama unajisi wa kutengwa kwake.
27 Na mtu ye yote atakayevigusa vitu vile atakuwa najisi, naye atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.
28 Lakini huyo mwanamke kwamba ametakaswa na kule kutoka damu kwake, ndipo atakapojihesabia siku saba, na baadaye atakuwa safi.
29 Siku ya nane atajipatia hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, na kumletea kuhani, mlangoni pa hema ya kukutania.
30 Kuhani atamsongeza mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana, kwa ajili ya kutoka damu ya unajisi kwake.
31 Ni hivi mtakavyowatenga wana wa Israeli na unajisi wao; ili wasife katika unajisi wao, hapo watakapoitia unajisi maskani yangu iliyo katikati yao.
32 Hii ndiyo sheria ya mwenye kisonono, na ya mtu ambaye shahawa yake yamtoka, akawa na unajisi kwa hiyo;
33 na ya mwanamke ambaye yu katika kutengwa kwake, na ya mtu ambaye ana kisonono, kama ni mtu mume, kama ni mtu mke, na ya huyo alalaye na mwanamke mwenye unajisi.