Mlango 25
1 Ibrahimu alioa mke mwingine jina lake akiitwa Ketura.
2 Akamzalia Zimrani, na Yokshani, na Medani, na Midiani, na Ishbaki, na Sua.
3 Yokshani akamzaa Sheba, na Dedani; na wana wa Dedani walikuwa Waashuri na Waletushi, na Waleumi.
4 Na wana wa Midiani walikuwa, Efa, na Eferi, na Hanoki, na Abida, na Eldaa. Hao wote walikuwa ni wana wa Ketura.
5 Ibrahimu akampa Isaka yote aliyokuwa nayo.
6 Lakini wana wa masuria aliokuwa nao Ibrahimu, Ibrahimu akawapa zawadi, naye akawaondoa katika mahali alipokaa Isaka mwanawe, wakati wa uhai wake, waende pande za mashariki, mpaka nchi ya Kedemu.
7 Hizi ndizo siku za miaka ya maisha ya Ibrahimu alizoishi, miaka mia, na sabini na mitano.
8 Ibrahimu akafariki, naye akafa katika uzee mwema, mzee sana, ameshiba siku, akakusanyika kwa watu wake.
9 Isaka na Ishmaeli wanawe wakamzika katika pango ya Makpela, katika shamba la Efroni bin Sohari Mhiti, lielekealo Mamre.
10 Katika lile shamba alilolinunua Ibrahimu kwa wazawa Hethi, huko ndiko alikozikwa Ibrahimu na Sara mkewe.
11 Ikawa, baada ya kufa kwake Ibrahimu, Mungu akambariki Isaka mwanawe. Naye Isaka akakaa karibu ya Beer-lahai-roi.
12 Hivi ndivyo vizazi vya Ishmaeli, mwana wa Ibrahimu, ambaye Hajiri, Mmisri, mjakazi wa Sara, alimzalia Ibrahimu.
13 Na haya ndiyo majina ya wana wa Ishmaeli, kwa majina yao, na kwa vizazi vyao. Mzaliwa wa kwanza wa Ishmaeli, ni Nebayothi, na Kedari, na Abdeeli, na Mibsamu,
14 na Mishma, na Duma, na Masa,
15 na Hadadi, na Tema, na Yeturi, na Nafishi, na Kedema.
16 Hao ndio wana wa Ishmaeli, na hayo ni majina yao, katika miji yao, na katika vituo vyao, maseyidi kumi na wawili kwa kufuata jamaa zao.
17 Na hii ndiyo miaka ya maisha ya Ishmaeli, miaka mia na thelathini na saba. Akakata roho, akafa, akakusanyika kwa watu wake.
18 Wakakaa toka Havila mpaka Shuri, unaoelekea Misri, kwa njia ya kwenda Ashuru. Akakaa katikati ya ndugu zake wote.
19 Na hivi ndivyo vizazi vya Isaka, mwana wa Ibrahimu. Ibrahimu alimzaa Isaka.
20 Isaka akawa mwenye miaka arobaini alipomtwaa Rebeka binti Bethueli, Mshami, wa Padan-aramu, ndugu wa Labani, Mshami, kuwa mke wake.
21 Isaka akamwomba Bwana kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye Bwana akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba.
22 Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza Bwana.
23 Bwana akamwambia,Mataifa mawili yamo tumboni mwako,Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako.Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili,Na mkubwa atamtumikia mdogo.
24 Siku zake za kuzaa zilipotimia, tazama! Mapacha walikuwamo tumboni mwake.
25 Wa kwanza akatoka, naye alikuwa mwekundu mwili wote kama vazi la nywele. Wakamwita jina lake Esau.
26 Baadaye ndugu yake akatoka, na mkono wake unamshika Esau kisigino. Akaitwa jina lake Yakobo. Isaka alikuwa mwenye miaka sitini mkewe alipowazaa.
27 Watoto wakakua, Esau alikuwa mtu ajuaye kuwinda wanyama, mtu wa nyikani, na Yakobo alikuwa mtu mtulivu, mwenye kukaa hemani.
28 Basi Isaka akampenda Esau, kwa sababu alikula mawindo yake, na Rebeka akampenda Yakobo.
29 Yakobo akapika chakula cha dengu. Esau akaja kutoka nyikani, naye alikuwa amechoka sana.
30 Esau akamwambia Yakobo, Tafadhali, unipe hicho chakula chekundu nile, kwa kuwa ninazimia mimi. Kwa hiyo walimwita jina lake Edomu.
31 Yakobo akamwambia, Kwanza niuzie leo haki yako ya mzaliwa wa kwanza.
32 Esau akasema, Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini haki hii ya uzazi?
33 Yakobo akamwambia, Uniapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza.
34 Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.