Mlango 10
1 Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari;
2 wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari;
3 wote wakala chakula kile kile cha roho;
4 wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo.
5 Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani.
6 Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani.
7 Wala msiwe waabudu sanamu, kama wengine wao walivyokuwa; kama ilivyoandikwa, Watu waliketi kula na kunywa, kisha wakasimama wacheze.
8 Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu ishirini na tatu elfu.
9 Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka.
10 Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika, wakaharibiwa na mharabu.
11 Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani.
12 Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.
13 Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.
14 Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu.
15 Nasema kama na watu wenye akili; lifikirini ninyi ninenalo.
16 Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo?
17 Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja.
18 Waangalieni hao Waisraeli walivyokuwa kwa jinsi ya mwili; wale wazilao dhabihu, je! Hawana shirika na madhabahu?
19 Basi niseme nini? Ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni kitu?
20 Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani.
21 Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani.
22 Au twamtia Bwana wivu? Je! Tuna nguvu zaidi ya yeye?
23 Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vifaavyo. Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vijengavyo.
24 Mtu asitafute faida yake mwenyewe, bali ya mwenzake.
25 Kila kitu kiuzwacho sokoni kuleni, bila kuuliza-uliza, kwa ajili ya dhamiri;
26 maana, Dunia ni mali ya Bwana na vyote viijazavyo.
27 Na mtu asiyeamini akiwaalika, nanyi mnataka kwenda, kuleni kila kitu kiwekwacho mbele yenu bila kuuliza-uliza, kwa ajili ya dhamiri.
28 Lakini mtu akiwaambia, Kitu hiki kimetolewa kiwe sadaka, msile, kwa ajili yake yeye aliyeonyesha, na kwa ajili ya dhamiri.
29 Nasema, dhamiri, lakini si yako, bali ya yule mwingine. Maana kwa nini uhuru wangu uhukumiwe na dhamiri ya mtu mwingine?
30 Ikiwa mimi natumia sehemu yangu kwa shukrani, kwa nini nitukanwe, kwa ajili ya kitu nikishukuriacho?
31 Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.
32 Msiwakoseshe Wayahudi wala Wayunani wala kanisa la Mungu,
33 vile vile kama mimi niwapendezavyo watu wote katika mambo yote, nisitake faida yangu mwenyewe, ila faida yao walio wengi, wapate kuokolewa.