Mlango 13
1 Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo.
2 Hata wakati wa chakula cha jioni; naye Ibilisi amekwisha kumtia Yuda, mwana wa Simoni Iskariote, moyo wa kumsaliti;
3 Yesu, hali akijua ya kuwa Baba amempa vyote mikononi mwake, na ya kuwa alitoka kwa Mungu naye anakwenda kwa Mungu,
4 aliondoka chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni.
5 Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga.
6 Hivyo yuaja kwa Simoni Petro. Huyo akamwambia, Bwana! Wewe wanitawadha miguu mimi?
7 Yesu akajibu, akamwambia, Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye.
8 Petro akamwambia, Wewe hutanitawadha miguu kamwe. Yesu akamwambia, Kama nisipokutawadha, huna shirika nami.
9 Simoni Petro akamwambia, Bwana, si miguu yangu tu, hata na mikono yangu na kichwa changu pia.
10 Yesu akamwambia, Yeye aliyekwisha kuoga hana haja ila ya kutawadha miguu, bali yu safi mwili wote; nanyi mmekuwa safi, lakini si nyote.
11 Kwa maana alimjua yeye atakayemsaliti; ndiyo maana alisema, Si nyote mlio safi.
12 Basi alipokwisha kuwatawadha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena, akawaambia, Je! Mmeelewa na hayo niliyowatendea?
13 Ninyi mwaniita, Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo.
14 Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi.
15 Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo.
16 Amin, amin, nawaambia ninyi, Mtumwa si mkuu kuliko bwana wake; wala mtume si mkuu kuliko yeye aliyempeleka.
17 Mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda.
18 Sisemi habari za ninyi nyote; nawajua wale niliowachagua; lakini andiko lipate kutimizwa, Aliyekula chakula changu Ameniinulia kisigino chake.
19 Tangu sasa nawaambia kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini ya kuwa mimi ndiye.
20 Amin, amin, nawaambieni, Yeye ampokeaye mtu ye yote nimpelekaye, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi; ampokea yeye aliyenipeleka.
21 Naye alipokwisha kusema hayo, Yesu alifadhaika rohoni, akashuhudia akisema, Amin, amin, nawaambieni, Mmoja wenu atanisaliti.
22 Wanafunzi wakatazamana, huku wakiona shaka ni nani amtajaye.
23 Na palikuwapo mmoja wa wanafunzi wake, ameegama kifuani pa Yesu, ambaye Yesu alimpenda.
24 Basi Simoni Petro akampungia mkono, akamwambia, Uliza, ni nani amtajaye?
25 Basi yeye, hali akimwelekea Yesu kifua chake, akamwambia, Bwana, ni nani?
26 Basi Yesu akajibu, Ndiye mtu yule nitakayemtowelea tonge na kumpa. Akatowelea tonge, akalitwaa akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskariote.
27 Na baada ya hilo tonge Shetani alimwingia. Basi Yesu akamwambia, Uyatendayo yatende upesi.
28 Wala hakuna mtu katika wale walioketi chakulani aliyeijua sababu ya kumwambia hivyo.
29 Kwa maana wengine walidhania, kwa kuwa Yuda huchukua mfuko, ya kwamba Yesu alimwambia kama, Nunua mnavyovihitaji kwa sikukuu; au kwamba awape maskini kitu.
30 Basi huyo, akiisha kulipokea lile tonge, akatoka mara hiyo. Nako kulikuwa ni usiku.
31 Basi huyo alipokwisha kutoka, Yesu alisema, Sasa ametukuzwa Mwana wa Adamu, naye Mungu ametukuzwa ndani yake.
32 Mungu naye atamtukuza ndani ya nafsi yake; naye atamtukuza mara.
33 Enyi watoto wadogo, bado kitambo kidogo nipo pamoja nanyi; mtanitafuta; na kama vile nilivyowaambia Wayahudi ya kwamba, Mimi niendako ninyi hamwezi kuja; kadhalika sasa nawaambia ninyi.
34 Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo.
35 Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.
36 Simoni Petro akamwambia, Bwana, unakwendapi? Yesu akamjibu, Niendako huwezi kunifuata sasa; lakini utanifuata baadaye.
37 Petro akamwambia, Bwana, kwa nini mimi nisiweze kukufuata sasa? Mimi nitautoa uhai wangu kwa ajili yako.
38 Yesu akamjibu, Je! Wewe utautoa uhai wako kwa ajili yangu? Amin, amin, nakuambia, Jimbi hatawika hata wewe utakapokuwa umenikana mara tatu.