Mlango 45
1 Tena, mtakapoigawanya nchi kwa kura iwe urithi, mtamtolea Bwana toleo, sehemu
takatifu ya nchi, urefu wake utakuwa urefu wa mianzi ishirini na tano elfu, na upana
wake elfu kumi; itakuwa takatifu ndani ya mipaka yake yote pande zote.
2 Katika hiyo itakuwako sehemu kwa mahali patakatifu, urefu wake mia tano, na upana
wake mia tano, mraba pande zote; na dhiraa ishirini kwa viunga vyake pande zote.
3 Na kwa kipimo hicho utapima, urefu wa ishirini na tano elfu, na upana wa elfu
kumi; na ndani yake patakuwa patakatifu, palipo patakatifu sana.
4 Hiyo ni sehemu takatifu ya nchi; itakuwa ya makuhani, wahudumu wa patakatifu,
wakaribiao kumhudumia Bwana; nayo itakuwa mahali kwa nyumba zao, na patakatifu kwa
mahali patakatifu.
5 Tena urefu wa ishirini na tano elfu, na upana wa elfu kumi, ni sehemu ya Walawi,
wahudumu wa nyumba, iwe milki yao wenyewe kwa vyumba ishirini.
6 Nanyi mtaiandika milki ya mji, upana wake elfu tano, na urefu wake ishirini na
tano elfu, kandokando ya mahali palipotolewa, iwe sehemu takatifu; nayo itakuwa ya
nyumba yote ya Israeli.
7 Na sehemu itakayokuwa ya mkuu itakuwa upande huu, na upande huu, wa toleo
takatifu, na wa milki ya mji, kulikabili toleo takatifu, na kuikabili milki ya mji,
upande wa magharibi kuelekea magharibi, na upande wa mashariki kuelekea mashariki; na
kwa urefu wake sawasawa na sehemu mojawapo, toka mpaka wa magharibi hata mpaka wa
mashariki.
8 Katika nchi hiyo itakuwa milki kwake katika Israeli; wala wakuu wangu
hawatawaonea watu wangu tena kabisa; bali watawapa nyumba ya Israeli nchi hiyo, kwa
kadiri ya makabila yao.
9 Bwana MUNGU asema hivi; Na iwatoshe ninyi, enyi wakuu wa Israeli; ondoeni dhuluma
na unyang'anyi; fanyeni hukumu na haki; ondoeni kutoza kwa nguvu kwenu katika watu
wangu, asema Bwana MUNGU.
10 Mtakuwa na mizani ya haki, na efa ya haki, na bathi ya haki.
11 Efa na bathi zitakuwa za kipimo kimoja; ili kwamba bathi ichukue sehemu ya kumi
ya homeri, na efa sehemu ya kumi ya homeri; kipimo chake kitakuwa kwa kadiri ya cheo
cha kawaida cha homeri.
12 Nayo shekeli itakuwa gera ishirini; shekeli tano zitakuwa shekeli tano, shekeli
kumi zitakuwa kumi, na shekeli hamsini zitakuwa mane yenu.
13 Toleo mtakalotoa ni hili; sehemu ya sita ya efa katika homeri moja ya ngano,
nanyi mtatoa sehemu ya sita ya efa katika homeri ya shayiri;
14 na sehemu ya mafuta iliyoamriwa, katika bathi ya mafuta, itakuwa sehemu ya kumi
ya bathi katika kori moja, ambayo ni bathi kumi, yaani homeri; maana bathi kumi ni
homeri moja;
15 na mwana-kondoo mmoja wa kundi katika mia mbili, katika malisho ya Israeli yenye
maji; kwa sadaka ya unga, na kwa sadaka ya kuteketezwa, na kwa sadaka za amani, ili
kuwafanyia upatanisho, asema Bwana MUNGU.
16 Watu wote wa nchi watatoa toleo hili kwa ajili ya mkuu katika Israeli.
17 Tena itakuwa kazi ya mkuu kutoa hizo sadaka za kuteketezwa, na sadaka za unga,
na sadaka za vinywaji, katika sikukuu, na katika mwezi mpya, na katika sabato, katika
sikukuu zote za nyumba ya Israeli zilizoamriwa; atatengeneza sadaka ya dhambi, na
sadaka ya unga, na sadaka ya kuteketezwa, na sadaka za amani, ili kufanya upatanisho
kwa ajili ya nyumba ya Israeli.
18 Bwana MUNGU asema hivi; Mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, utatwaa
ng'ombe mchanga mume mkamilifu; nawe utapatakasa mahali patakatifu.
19 Na kuhani atatwaa baadhi ya damu ya sadaka ya dhambi, na kuitia juu ya miimo ya
milango ya nyumba, na juu ya pembe nne za daraja ya madhabahu, na juu ya miimo ya
lango la ua wa ndani.
20 Nawe utafanya vivyo hivyo katika mwezi wa saba, siku ya kwanza ya mwezi kwa
ajili ya kila mtu akosaye, na kwa ajili ya mtu aliye mjinga, ndivyo mtakavyoifanyia
nyumba upatanisho.
21 Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi, mtakuwa na Pasaka, sikukuu ya
siku saba; mkate usiotiwa chachu utaliwa.
22 Na siku hiyo mkuu atatengeneza ng'ombe kuwa sadaka ya dhambi, kwa ajili ya nafsi
yake, na kwa ajili ya watu wote wa nchi.
23 Tena, katika zile siku saba za sikukuu atamtengenezea Bwana sadaka ya
kuteketezwa, ng'ombe saba na kondoo waume saba wakamilifu, kila siku kwa muda wa siku
saba, na beberu mmoja kila siku kuwa sadaka ya dhambi.
24 Naye atatengeneza sadaka ya unga, efa moja kwa ng'ombe, na efa moja kwa kondoo
mume, na hini moja ya mafuta kwa efa moja;
25 katika mwezi wa saba, siku ya kumi na tano ya mwezi, katika sikukuu atafanya
vivyo hivyo kwa muda wa siku saba; sadaka ya dhambi vivyo hivyo, na sadaka ya
kuteketezwa vivyo hivyo, na sadaka ya unga vivyo hivyo, na mafuta vivyo hivyo.