Mlango 21
1 Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala; akatawala miaka hamsini na mitano katika Yerusalemu, na jina la mamaye aliitwa Hefziba.
2 Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, sawasawa na machukizo ya mataifa, aliowafukuza Bwana mbele ya wana wa Israeli.
3 Kwa maana akapajenga tena mahali pa juu alipopaharibu Hezekia baba yake; akamjengea Baali madhabahu, akafanya Ashera kama alivyofanya Ahabu mfalme wa Israeli. Akajiinama mbele ya jeshi lote la mbinguni na kulitumikia.
4 Akazijenga madhabahu ndani ya nyumba ya Bwana, napo ndipo alipopanena Bwana, Katika Yerusalemu nitaliweka jina langu.
5 Akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni katika behewa mbili za nyumba ya Bwana.
6 Akampitisha mwanawe motoni, akatazama bao, akafanya uganga, akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, na wachawi; akafanya mabaya mengi machoni pa Bwana, hata kumkasirisha.
7 Akaiweka sanamu ya kuchongwa ya Ashera aliyoifanya ndani ya nyumba, ambayo Bwana alimwambia Daudi, na Sulemani mwanawe, Katika nyumba hii, na katika Yerusalemu, niliouchagua miongoni mwa kabila zote za Israeli, nitaliweka jina langu milele;
8 wala sitawapotosha Israeli miguu watoke katika nchi niliyowapa baba zao; wakiangalia tu na kufanya sawasawa na yote niliyowaamuru, na kwa kuishika torati yote aliyowaamuru mtumishi wangu Musa.
9 Walakini hawakusikia; naye Manase akawakosesha wafanye mabaya, kuliko mataifa Bwana aliowaharibu mbele za wana wa Israeli.
10 Bwana akanena kwa watumishi wake manabii, akisema,
11 Kwa sababu Manase mfalme wa Yuda amefanya machukizo haya, na kutenda vibaya kuliko yote waliyoyatenda Waamori, waliokuwa kabla yake, naye akawakosesha Yuda kwa sanamu zake;
12 kwa sababu hiyo Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Angalia, naleta mabaya juu ya Yerusalemu na juu ya Yuda, hata kila mtu asikiaye, masikio yake yatawasha yote mawili.
13 Nami nitanyosha juu ya Yerusalemu kamba ya Samaria, na timazi ya nyumba ya Ahabu; nami nitaifuta Yerusalemu, kama mtu afutavyo sahani, kuifuta na kuifudikiza.
14 Nami nitawatupa mabaki ya urithi wangu, na kuwatia mikononi mwa adui zao; nao watakuwa nyara na mateka kwa adui zao wote;
15 kwa sababu wametenda yaliyo mabaya machoni pangu, na kunikasirisha, tangu siku ile walipotoka baba zao katika Misri, hata leo hivi.
16 Na Manase akazimwaga damu zisizo na hatia, nyingi sana, hata alipokuwa ameijaza Yerusalemu tangu upande huu hata upande huu; zaidi ya kosa lake alilowakosesha Yuda, kutenda yaliyo mabaya machoni pa Bwana.
17 Basi mambo yote ya Manase yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na kosa lake alilolikosa, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
18 Manase akalala na babaze, akazikwa katika bustani ya nyumba yake mwenyewe, yaani, bustani ya Uza. Na Amoni mwanawe akatawala mahali pake.
19 Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala; akatawala miaka miwili huko Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Meshulemethi, binti Haruzi wa Yotba.
20 Akafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana, kama Manase babaye alivyofanya.
21 Akaiendea njia yote aliyoiendea baba yake, akazitumikia sanamu alizozitumikia baba yake, akaziabudu.
22 Akamwacha Bwana, Mungu wa babaze, wala hakuiendea njia ya Bwana.
23 Nao watumishi wa Amoni wakafanya fitina juu yake, wakamwua mfalme ndani ya nyumba yake mwenyewe.
24 Lakini watu wa nchi wakawaua wote waliofanya fitina juu yake mfalme Amoni, watu wa nchi wakamfanya Yosia mwanawe awe mfalme mahali pake.
25 Basi mambo yote ya Amoni yaliyosalia, aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
26 Akazikwa kaburini mwake katika bustani ya Uza. Na Yosia mwanawe akatawala mahali pake.