Mlango 8
1 Bwana akamwambia Musa, Ingia kwa Farao, ukamwambie, Bwana asema hivi, Wape watu wangu ruhusa, ili wapate kunitumikia.
2 Tena kama ukikataa kuwapa ruhusa, tazama, nitaipiga mipaka yako yote kwa kuleta vyura;
3 na huo mto utafurika vyura, nao watakwea juu na kuingia ndani ya nyumba yako, na ndani ya chumba chako cha kulala, na juu ya kitanda chako, na ndani ya nyumba ya watumishi wako, na juu ya watu wako, na ndani ya meko yako, na ndani ya vyombo vyako vya kukandia unga.
4 Kisha hao vyura watakwea juu yako wewe, na juu ya watu wako, na juu ya watumishi wako wote.
5 Bwana akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha mkono wako na fimbo yako juu ya mito, juu ya vijito, na juu ya maziwa ya maji, ukawalete vyura waje juu ya nchi yote ya Misri.
6 Basi Haruni akaunyosha mkono wake juu ya maji yote ya Misri; na hao vyura wakakwea juu, wakaifunika nchi ya Misri.
7 Waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao; na kuwaleta vyura juu ya nchi ya Misri.
8 Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni na kuwaambia, Mwombeni Bwana, ili awaondoe vyura hawa kwangu mimi na kwa watu wangu; nami nitawapa watu ruhusa waende zao, ili wamtolee Bwana dhabihu.
9 Musa akamwambia Farao, Haya, ujitukuze juu yangu katika jambo hili; sema ni lini unapotaka nikuombee wewe, na watumishi wako, na watu wako, ili hao vyura waangamizwe watoke kwako wewe na nyumba zako, wakae ndani ya mto tu.
10 Akamwambia, Kesho, Akasema, Na yawe kama neno lako; ili upate kujua ya kwamba hapana mwingine mfano wa Bwana, Mungu wetu.
11 Hao vyura wataondoka kutoka kwako wewe na nyumba zako, na watumishi wako, na watu wako; watasalia mtoni tu.
12 Basi Musa na Haruni wakatoka kwa Farao; Musa akamlilia Bwana katika jambo la hao vyura aliokuwa amewaleta juu ya Farao.
13 Bwana akafanya sawasawa na neno la Musa; na hao vyura wakafa kutoka katika zile nyumba, na katika viwanja, na katika mashamba.
14 Wakawakusanya chungu chungu; na nchi ikatoa uvundo.
15 Lakini Farao alipoona ya kuwa pana nafuu, akaufanya moyo wake kuwa mzito, asiwasikize; kama Bwana alivyonena.
16 Bwana akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha fimbo yako, ukayapige mavumbi ya nchi, ili kwamba yawe chawa katika nchi yote ya Misri.
17 Nao wakafanya; Haruni akaunyosha mkono wake na fimbo yake, na kuyapiga mavumbi ya nchi, nayo yakawa chawa juu ya wanadamu na juu ya wanyama; mavumbi yote ya nchi yakawa ni chawa katika nchi yote ya Misri.
18 Hao waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao, ili kwamba walete chawa, lakini wasiweze; nako kulikuwa na chawa juu ya wanadamu, na juu ya wanyama.
19 Ndipo wale waganga wakamwambia Farao, Jambo hili ni chanda cha Mungu; na moyo wake Farao ukawa mgumu asiwasikize; vile vile kama Bwana alivyonena.
20 Bwana akamwambia Musa, Inuka asubuhi na mapema usimame mbele ya Farao; angalia! Atoka aende majini; kamwambie, Bwana asema, Wape watu wangu ruhusa waende zao, ili wanitumikie mimi.
21 Au kwamba huwapi ruhusa watu wangu, tazama, nitaleta wingi wa mainzi juu yako wewe, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako, nao wataingia ndani ya nyumba zako; na nyumba za Wamisri zitajawa na wingi wa mainzi, na nchi nayo ambayo wa juu yake.
22 Nami siku hiyo nitatenga nchi ya Gosheni, watu wangu wanayokaa, ili hao mainzi wasiwe huko; ili kwamba upate kujua wewe ya kuwa mimi ndimi Bwana kati ya dunia.
23 Nami nitatia mpaka kati ya watu wangu na watu wako; ishara hiyo italetwa kesho.
24 Bwana akafanya; wakaja wingi wa mainzi kwa uzito sana, wakaingia nyumbani mwa Farao, na katika nyumba za watumishi wake, tena katika nchi yote ya Misri; nayo nchi iliharibiwa kwa ajili ya wale mainzi.
25 Farao akawaita Musa na Haruni akawaambia, Endeni mkamtolee Mungu wenu dhabihu ndani ya nchi hii.
26 Musa akasema, Haitupasi kufanya hivyo; kwa kuwa tutamchinjia sadaka Bwana, Mungu wetu, na hayo machukizo ya Wamisri; je! Tutachinja sadaka ya hayo machukizo ya Wamisri mbele ya macho yao, wasitupige kwa mawe?
27 La, tutakwenda safari ya siku tatu jangwani, tumchinjie dhabihu Bwana, Mungu wetu, kama atakavyotuagiza.
28 Farao akasema, Mimi nitawapa ruhusa mwende, ili mmchinjie dhabihu Bwana, Mungu wenu, jangwani; lakini hamtakwenda mbali sana; haya niombeeni.
29 Musa akasema, Tazama, mimi natoka kwako, nami nitamwomba Bwana ili hao mainzi wamtoke Farao, na watumishi wake, na watu wake kesho; lakini Farao asitende kwa udanganyifu tena, kwa kutowaacha watu waende kumchinjia Bwana dhabihu.
30 Musa akatoka kwa Farao, akamwomba Bwana.
31 Bwana akafanya kama neno la Musa, akawaondoa wale mainzi wabaya kwake Farao, na kwa watumishi wake, na watu wake; hakusalia hata mmoja.
32 Farao akaufanya moyo wake kuwa mzito mara hiyo nayo, wala hakuwapa ruhusa hao watu waende zao.