Mlango 41
1 Akanileta mpaka hekaluni, akaipima miimo, upana wake dhiraa sita upande mmoja, na
upana wake dhiraa sita upande wa pili, ambao ulikuwa ni upana wa maskani.
2 Na upana wa maingilio yake ulikuwa dhiraa kumi; na mbavu za maingilio zilikuwa
dhiraa tano upande huu, na dhiraa tano upande huu; akaupima urefu wake, dhiraa
arobaini, na upana wake, dhiraa ishirini.
3 Kisha akaingia ndani, akapima kila mwimo wa maingilio, dhiraa mbili; nayo
maingilio, dhiraa sita; na upana wa maingilio dhiraa saba.
4 Akaupima urefu wake; dhiraa ishirini, na upana wake, dhiraa ishirini, mbele ya
hekalu; akaniambia, Hapa ndipo mahali patakatifu kuliko kila mahali.
5 Kisha akaupima ukuta wa nyumba, dhiraa sita; na upana wa kila chumba cha mbavuni,
dhiraa nne, kuizunguka nyumba pande zote.
6 Na vile vyumba vya mbavuni vilikuwa na orofa tatu, moja juu ya mwenziwe; vilikuwa
thelathini, safu baada ya safu; navyo viliingia ndani ya ukuta uliokuwa wa nyumba, kwa
vile vyumba vya mbavuni pande zote vipate kushikamana nao, wala visishikamane na ukuta
wa nyumba.
7 Na vile vyumba vya mbavuni vilizidi kuwa vipana, kwa kadiri vilivyoizunguka
nyumba juu kwa juu; maana kule kuzunguka kwake kulikwenda juu kwa juu, kuizunguka
nyumba; basi upana wa nyumba ulikuwa ule ule hata juu; basi hupanda juu toka chumba
cha chini hata chumba cha juu, kwa njia ya kile chumba cha katikati.
8 Tena, nikaona ya kwamba nyumba ile ilikuwa na sakafu ya mawe, iliyoinuliwa pande
zote; nayo misingi ya vyumba vya mbavuni ilikuwa mwanzi mzima wa dhiraa sita.
9 Unene wa ukuta uliokuwa wa vile vyumba vya mbavuni, upande wa nje, ulikuwa dhiraa
tano; nayo nafasi iliyobaki ilikuwa dhiraa tano; na kati ya vyumba vya mbavuni vya
nyumba,
10 na vyumba vya walinzi, upana wa dhiraa ishirini, kuizunguka nyumba pande zote.
11 Na milango ya vile vyumba vya mbavuni iliielekea nafasi ile iliyobaki, mlango
mmoja ulielekea upande wa kaskazini, na mlango mmoja upande wa kusini; na upana wa
nafasi iliyobaki ulikuwa dhiraa tano pande zote.
12 Nalo jengo lililokabili mahali palipotengeka upande wa magharibi, upana wake
dhiraa sabini; na ukuta wa lile jengo, unene wake dhiraa tano pande zote, na urefu
wake dhiraa tisini.
13 Basi akaipima nyumba, urefu wake dhiraa mia; na mahali pale palipotengeka na
jengo lile, pamoja na kuta zake, urefu wake dhiraa mia;
14 tena upana wa uso wa nyumba, na wa mahali palipotengeka upande wa mashariki,
dhiraa mia.
15 Akaupima urefu wa jengo lile lililokabili mahali palipotengeka, palipokuwa nyuma
yake, na baraza zake upande huu na upande huu, dhiraa mia; na hekalu la ndani, na
kumbi za ua;
16 na vizingiti, na madirisha yaliyofungwa, na baraza za pande zote za orofa zile
tatu, zilizokikabili kizingiti, zilitiwa mabamba ya mti pande zote; na toka chini hata
madirishani; (nayo madirisha yamefunikwa);
17 na mpaka juu ya mlango hata nyumba ya ndani, na nje, na juu ya kuta zote pande
zote, katika nyumba ya ndani, na ya nje,
18 kulipambwa kwa makerubi na mitende; mtende mmoja kati ya kerubi na kerubi, na
kila kerubi lilikuwa na nyuso mbili;
19 basi palikuwa na uso wa mwanadamu kuelekea mtende mmoja, na uso wa mwana-simba
kuelekea mtende wa pili; ndivyo vilivyofanyika katika nyumba nzima pande zote.
20 Toka chini hata juu ya mlango makerubi yamefanyika, na mitende, na vivi hivi
ukuta wa hekalu.
21 Na hilo hekalu, miimo ya milango yake ilikuwa ya miraba; na mbele ya patakatifu
kuonekana kwake palionekana kama hapo kwanza.
22 Madhabahu ilikuwa ni ya miti, kimo chake dhiraa tatu, na urefu wake dhiraa
mbili; na pembe zake, na msingi wake, na kuta zake zilikuwa za miti; akaniambia, Hii
ndiyo meza iliyo mbele za Bwana.
23 Nalo hekalu na patakatifu palikuwa na milango miwili.
24 Na milango hiyo, kila mmoja ulikuwa na mbao mbili; mbao mbili zigeukazo; mbao
mbili za mlango mmoja, na mbao mbili za mlango wa pili.
25 Na milango ya hekalu ilifanyiziwa makerubi na mitende vile vile, kama zile kuta
zilivyofanyiziwa; tena palikuwa na boriti nene juu ya uso wa ukumbi, nje.
26 Tena palikuwa na madirisha yaliyofungwa, na mitende, upande huu na upande huu,
katika pande za ukumbi; ndiyo habari ya vyumba vya mbavuni vya nyumba hiyo, na vya
boriti zile nene.